Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kazi imeanza, Simba, Yanga kila mtu kivyake

Paziaaa Kazi imeanza, Simba, Yanga kila mtu kivyake

Fri, 16 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Game On! Sasa kazi inaanza rasmi. Ligi Kuu Bara inaanza leo Ijumaa, lakini kesho kuna mechi nyingine nne za ligi hiyo ukiwamo ule wa Simba dhidi ya Tabora United sambamba na michezo ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika. Lakini hata katika Klabu Bingwa kwa nchi za Cecafa nako ‘game on’ huko Ethiopia.

Yanga, Azam FC na Coastal Union ambazo hazitacheza mechi za Ligi Kuu kwa wikiendi hii, zenyewe zipo bize na mechi za raundi ya kwanza, kama itakavyokuwa kwa wawakilishi wa Zanzibar, JKU na Uhamiaji, huku mnyama akisubiri hadi raundi ya pili ya michuano hiyo ya ubingwa wa Afrika kwa ngazi za klabu.

Simba Queens ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Cecafa kusaka tiketi ya Klabu Bingwa Afrika itakuwa uwanjani keshokutwa Jumapili dhidi ya FAD ya Djibouti, licha ya michuano hiyo kuanza rasmi leo ikishirikisha klabu tisa tofauti zilizofangwa makundi mawili.

PAMBA VS PRISONS

Tuanze na Ligi Kuu. Baada ya tambo na maandalizi ya msimu mpya, ikiwamo usajili na kutesti mitambo, sasa mambo yatakuwa hadharani kujua nani alifanya nini, wakati ligi hiyo ikianza kwa mchezo mmoja tu kati ya Pamba Jiji iliyopanda daraja kutoka Ligi ya Championship na maafande wa Tanzania Prisons.

Mechi hiyo ya ufunguzi wa ligi hiyo kwa msimu wa 2024-2025 itapigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya kesho Jumamosi na keshokutwa Jumapili kupigwa michezo mingine minne ukiwamo wa Mnyama, Simba itakayoanza nyumbani dhidi ya Tabora United.

Pamba na Prisons zilizowahi kutikisa soka la Tanzania miaka ya 1990 kabla ya kupoteza uelekeo, zinakutana katika mchezo huo wa kwanza, huku kazi kubwa ikiwa kwa Wana TP Lindanda waliorudi katika ligi hiyo baada ya msoto wa zaidi ya miaka 20 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001.

Pamba imepanda daraja msimu huu ikiwa sambamba na KenGold itakayoanza msimu kwa kuialika Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Nyota wa timu hizo mbili yaani Pamba na Tanzania Prisons watakuwa na kazi ya kutaka kuvunja rekodi ya msimu uliopita ya bao la kwanza la msimu, iliyowekwa na Elias Maguri wa Geita Gold iliyoshuka daraja ambaye alifunga dhidi ya Ihefu alipofunga katika dakika ya tano wakati Geita ikishinda 1-0.

Bao hilo ndilo alililomaliza nalo nyota huyo wa zamani wa Prisons, Ruvu Shooting, Simba, Stand United na KMC, kwani hakufunga tena hadi msimu ulipoisha Mei 28 mwaka huu.

Pamba licha ya ugeni iliyonayo katika ligi hiyo baada ya miaka zaidi ya 20 tangu iliposhuka, imefanya usajili mkubwa unaotoa picha Prisons ijiandae kukabiliana na kazi nzito, kwani wageni hao wana George Mpole Mfungaji Bora wa ligi hiyo msimu wa 2021-2022 enzi akiwa na Geita akifunga mabao 17, ni mzoefu wa ligi, hivyo mabeki wa Prisons wanatakiwa kumchunga ili kuepusha madhara langoni mwao, japo taarifa zinasema huenda akaukosa mchezo huo kwa kutokuwa fiti kimwili.

Ukiachana na Mpole, timu hiyo pia ina vifaa vya maana kama Ben Nakibinge, Eric Okutu, Samuel Atwi, Samson Madeleke, Ally Ramadhan ‘Oviedo’ (Mashujaa) na Kenneth Kunambi ambao ni wazoefu wakubwa wa ligi hiyo mbali na nyota wa kigeni iliowasajili chini ya kocha mzoefu wa ligi ya Bara, Goran Kopunovic.

Kwa upande wa Prisons, iliyomaliza nafasi ya tisa msimu uliopita ikivuna pointi 34 ina faida ya kuwa na wachezaji wanaoifahamu Pamba nje ndani, kama Ismail Ally, Haruna Chanongo walioshiriki kuipandisha kabla ya kuhama, lakini wenyewe ni timu zoefu wa ligi hiyo na huwa haitabiriki.

Prisons nayo imefanya usajili nzuri kwa kuwarudisha baadhi ya nyota wao wa zamani na wazoefu wa ligi hiyo kama kipa Samson Sebusebu, Seleman Ibrahim ‘Boban’, (Geita Gold), Oscar Mwajanga (Mbeya Kwanza), Abubakar Ngalema, Meshack Abraham (Dodoma Jiji), Vedastus Mwihambi, Ezekia Mwashilindi (Singida BS), Wema Sadoki (JKT TZ) ikiwa chini ya kocha anayeijua Pamba, Mbwana Makatta aliyeipandisha.

Kocha wa Pamba, Goran Kopunovic alisema maandalizi yamekamilika na wachezaji wake wote kwa asilimia kubwa wapo tayari kuipambania timu kuhakikisha inaanza vizuri kwenye uwanja wake wa nyumbani.

“Wachezaji wangu sio wageni wa ligi, timu ndiyo imepanda lakini nina wachezaji wengi ambao wamecheza ligi kwa muda mrefu hivyo natarajia mchezo mzuri na wa ushindani kutoka kwa wapinzani wangu nitaingia kwa kuwaheshimu lengo ni kupata pointi tatu.”

Kocha wa Prisons, Mbwana Makatta alisema wamefanya maandalizi vizuri na wapo tayari kuikabili Pamba na amesisitiza ni timu nzuri itakayowapa ushindani na watacheza kwa kuwaheshimu.

“Pamba imepanda daraja msimu huu hicho hakiwezi kuwa kigezo cha sisi kubweteka tutaingia kupambana dakika zote 90 lengo ni kuona tunapata mchezo mzuri na pointi tatu ugenini,” alisema.

KESHO MECHI MBILI

Ukiachana na mechi hiyo ya kukata utepe wa msimu huu, kesho kutapigwa mechi nyingine mbili na Mashujaa itaialika Dodoma Jiji zote zikitoka kufanya usajili wa kishindo sambamba na pre season za maana na kubwa zina wachezaji wanaofahamiana.

Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya saa 1:00 usiku Namungo kuialika Fountain Gate Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi.

Keshokutwa Jumapili itakuwa ni zamu ya KenGold na Singida BS zitakazoumana saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya na mara baada ya mechi hiyo washindi namba tatu wa msimu uliopita na wa Ngao ya Jamii msimu huu, Simba itashuka Uwanja wa KMC Complex, kuvaana na Tabora United.

Mechi zote hizo zitakuwa ni kipimo kizuri kwa timu hizo kutokana na usajili ilizofanya huku, Simba ikiwa na kazi kubwa ya kuthibitisha, msimu huu wapo vizuri chini ya kocha Fadlu Davids anayeiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza katika ligi hiyo akitokea Raja Casablanca ya Morocco.

Kila timu inapiga hesabu a kuanza hesabu vyema kwa kusaka pointi tatu, lakini kwa Fadlu kutaka kuonyesha kuwa ana kitu kipya alichowaletea Wanamsimbazi ambao msimu uliopita walitoka kapa katika ligi hiyo na Kombe la Shirikisho sambamba na Ligi ya Mabingwa Afrika iliyomaliza hatua ya robo fainali.

Tabora iliyonusurika kushuka daraja kupitia mechi za play-off yenyewe haitapenda kuanza ligi hiyo ya msimu wa pili kwa aibu kama ilivyokuwa msimu uliopita ilipokandikwa mabao 4-1 na Azam FC ikiwa na wachezaji pungufu, kwani safari hii wamekisuka upya kikosi hicho na kuwa na mashine za maana za kuitesti Simba.

KIMATAIFA

Wakati Simba ikianza kuliamsha katika Ligi Kuu, vigogo wenzake, Azam FC, Yanga pamoja na Coastal sawia na JKU na Uhamiaji za Zanzibar zenyewe zitakuwa na kibarua cha mechi za kimataifa, wakati zitakapotupa karata ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho zikiwa nyumbani na ugenini. Mechi hizo za kimataifa zinaanza rasmi Ijumaa hii, lakini kwa wawakilishi wa Tanzania kazi itaanza rasmi kesho.

Yanga ndiyo itakayokata utepe kwa anga hizo kwa kucheza na Vital’O ya Burundi ambao ndio wenyeji kwenye Uwanja wa Azam Complex, kuanzia saa 10:00 jioni kabla ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union inayorejea katika michuano hiyo tangu 1989, itakuwa ugenini kuvaana na Bravos do Maquis ya Angola saa 12:00 jioni, kisha ngoma nyingine tatu zitapigwa Jumapili, Uhamiaji ikiamsha mapema.

Uhamiaji ambao ni wenyeji wa mchezo huo itakuwa Libya kupepetana na Al Ahli Tripoli kuanzia saa 9:30, alasiri katika mechi ya Kombe la Shirikisho, kabla ya Azam na JKU kufuata katika Ligi ya Mabingwa.

Azam itakuwa wenyeji wa APR ya Rwanda kuanzia saa 12:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex, kabla ya JKU itakuwa wenyeji wa Pyramids ya Misri mechi itakayopigwa jijini Cairo saa 2:00 usiku timu hizo zikitesti zali baada ya kuchemsha msimu uliopita katika Kombe la Shirikisho zikitolewa raundi za mapema.

JKU ilitolewa na Singida BS, wakati Azam iling’olewa na Wahabeshi wa Bahir Dar Kenema kwa njia ya matuta na safari hii zinatesti zali katika Ligi ya Mabingwa ambao Yanga chini ya Gamondi iliweka rekodi kwa kuingia makundi baada ya kupita miaka 25 tangu ilipofanya hivyo mwaka 1998 na kwenda hadi robo.

Safari hii Yanga ikiwa na mziki mnene wa nyota waliokuwa msimu uliopita na wale waliongezwa akiwamo Clatous Chama, Jean Baleke, Duke Abuya wazoefu wa michuano hiyo sambamba na kina Chadrack Boka na Abubakar Khomeiny wana kiu ya kuisimamisha Vital’O ambao sio wageni kwa soka la Tanzania.

Mara baada ya mechi za wikiendi hii, timu hizo tano zitashuka tena uwanjani kwenye michezo ya marudiano wikiendi ijayo ili kuwania kutinga raundi ya pili ambako Simba inayoshiriki Kombe la Shirikisho itaanzia hapo dhidi ya mshindi wa mechi ya Uhamiaji na Al Ahli Tripoli ili kusaka tiketi ya kutinga makundi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: