Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kadi ya kocha yaivusha Denmark mtoano Euro 2024

Slovenia Denmark Kadi ya kocha yaivusha Denmark mtoano Euro 2024

Thu, 27 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Denmark imeibwaga Slovenia kwenye vita ya kugombea nafasi ya pili kwenye Kundi C la fainali za Euro 2024 huko Ujerumani.

Timu hizo mbili zilitoka sare kwenye mechi zao zote za hatua ya makundi ya fainali hizo za Euro 2024, hivyo kila moja kumaliza na pointi tatu, mbili nyuma ya vinara England.

Si hivyo tu, bali timu hizo zilitoka sare ya 1-1 zilipokutana zenyewe, huku mechi zao nyingine zilikuwa za matokeo ya 1-1 na 0-0 katika za mwisho za makundi, ambapo Denmark ilicheza na Serbia na Slovenia ilikipiga na England.

Hiyo ina maana timu zote hizo tofauti ya mabao ni 0, ambapo zimefunga mabao mawili na zimefungwa mabao mawili. Kwa maana hiyo, kama Denmark na Slovenia zingekuwa zimecheza mechi ya mwisho, basi zingehitaji mikwaju ya penalti kupata mshindi.

Lakini, kuna kanuni ndogo iliyotumika kupata timu ya kushika nafasi ya pili baada ya mlingano huo. Na kilichotazamwa ni rekodi ya nidhamu ya timu hizo kwenye fainali za Euro 2024. Mwanzoni kulikuwa na mkanganyiko wa kuhusu nidhamu ya timu hizo, maana Slovenia na Denmark zote zina wachezaji sita walioonyeshwa kadi za njano kwenye fainali hizo za Ujerumani katika mechi hizo tatu.

Hata hivyo, kilichoiponza Slovenia ni mmoja wa makocha wake ambapo kocha msaidizi Milivoje Novakovic, alionyeshwa kadi ye njano katika mechi ya kwanza ilipokumbana na Denmark. Hiyo ina maana kwenye ishu ya nidhamu, Denmark ilikuwa na kadi sita na Slovenia saba.

Kama Novakovic asingekuwa ameonyeshwa kadi ya njano, basi mambo yangekuwa sawa pia hadi kwenye ishu ya nidhamu na hapo, basi Uefa ingatazama rekodi ya mechi za kufuzu fainali za Euro 2024.

Uzuri timu zote zilikuwa kwenye kundi moja la mechi za kufuzu na zilimaliza na pointi 22, zikishinda saba, sare moja na vichapo viwili.

Slovenia ilikuwa na tofauti nzuri ya mabao, lakini Denmark ilikuwa juu kwenye mechi za wenyewe kwa wenyewe. Mechi iliyofanyika Slovenia, Juni 2023 ilimalizika kwa sare ya 1-1, lakini ile ya Denmark mwenyewe alishinda 2-1 huko Copenhagen, Novemba.

Kutokana na hilo, Denmark ilifuzu fainali za Euro ikishika namba tisa kwenye viwango, wakati Slovenia ikiwa namba 15. Lakini, kwenye kupata timu ya kushika namba mbili kwenye Kundi C, kadi ya njano ya kocha msaidizi wa Slovenia ilimaliza utata na kuibeba Denmark.

Hata hivyo, jambo hilo limeiweka Denmark kwenye msala mkubwa kwani itakabiliana na Ujerumani kwenye hatua ya 16 bora.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: