Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Joto la Euro 2024... Les Bleus ni shida

France Les Blues Joto la Euro 2024... Les Bleus ni shida

Sat, 15 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

JOTO limezidi kupamba moto kwenye fainali za Euro 2024 huku kila taifa likipambana kuhakikisha linaanza vizuri kwenye mechi zao za kwanza za mikikimikiki hiyo iliyoanza jana Ijumaa huko Ujerumani.

Leo, Jumamosi zitapigwa mechi tatu, ambapo mapema kabisa, Hungary itakuwa na kibarua kizito cha kuikabili Uswisi, kabla ya mashabiki kushuhudia mechi ya kibabe sana, wakati Hispania itakapoonyeshana ubabe na Croatia na baada ya hapo, Italia inaingia mzigoni pia kukipiga na Albania. Mambo ni moto.

Hata hivyo, presha ipo huko kwenye kambi ya Ufaransa baada ya supastaa wao, Kylian Mbappe kushindwa kufanya mazoezi kutakana na kunaswa na virusi vya mafua. Kinachoelezwa ni kwamba kikosi hicho cha kocha Didier Deschamps kinachofahamika kama Les Bleus kimekumbwa na balaa la mastaa wake kuambukizwa mafua na hivyo kuweka wasiwasi kama watakuwa fiti kucheza kwenye mechi yao ya kwanza kwenye michuano hiyo.

Mbappe, 25, ambaye ni nahodha wa Ufaransa ni moja kati ya mastaa wawili wa kikosi hicho waliokosa mazoezi ya wazi huko Paderborn, ambapo mchezaji mwingine ambaye hakufanya mazoezi na wenzake ni winga wa Bayern Munich, Kingsley Coman.

Coman alikosekana kutokana na kuugua, wakati Mbappe alijitenga na kufanya mazoezi ya kivyake huko gym baada ya kupata dakika chache sana alizofanya mazoezi na wenzake tangu kikosi hicho kilipokutana kambini Paris, Ufaransa mwezi uliopita.

Kumekuwa na imani kwmaba huenda Mbappe hakunaswa na virusi hivyo vya mafanio, lakini kitendo cha kufanya mazoezi peke yake na kujitenga na wenzake kumeibua zaidi hofu. Ufaransa itarusha kete yake ya kwanza kwenye fainali hizo kwa kumenyana na Austria huko Dusseldorf, Jumatatu.

Wachezaji kibao wamekuwa wakisumbuliwa na mafua kwenye kikosi hicho cha Ufaransa kabla ya kwenda Ujerumani kwenye fainali hizo za Euro 2024. Winga, Ousmane Dembele, anayekipiga kwenye kikosi cha Paris Saint-Germain, alifichua kusumbuliwa na mafua, lakini anaamini ataweza kupona kwa wakati na kuitumikia timu yake kwenye mechi ya kwanza ya michuano hiyo.

Dembele alisema: “Kwa upande wangu, naendelea vizuri. Nilikuwa na mafua wiki iliyopita na nilikuwa wa kwanza, lakini najisikia vizuri kwa sasa.

“Timu ipo vizuri. Kila mtu atakuwa fiti ndani ya siku chache zijazo.”

Kocha Didier Deschamps naye aliripotiwa kuambukizwa mafua. Kikosi cha Ufaransa kilifanya mazoezi ya wazi mbele ya mashabiki 4,000 huko Paderborn. Tiketi kwa mashabiki waliokwenda kutazama mazoezi hayo, zilimalizika ndani ya dakika chache tu.

Deschamps na kikosi chake kimepokea kwa shangwe kubwa huko Ujerumani kilipowasili Jumatano iliyopita, ambapo wimbo wa taifa wa Ufaransa uliimbwa kabla ya mashabiki kujipanga kuwashangilia mastaa wa timu hiyo karibu na hoteli yao Bad Lippspringe.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: