Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Jobe apata shavu CAF

Pa Omar Jobe Rrrrr Pa Omar Jobe

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Siku chache baada ya kutemwa na Simba, mshambuliaji Pa Omar Jobe amekula shavu kwa kusajiliwa na klabu ya Nouadhibou FC ya Mauritania itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, tofauti Wekundu wa Msimbazi ambao watacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba ilipoteza nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa iliyoshiriki misimu sita mfululizo na kufika robo fainali mara nne baada ya kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu Bara nyuma ya Yanga na Azam zilizokata tiketi ya michuano hiyo mikubwa na yenye mkwanja wa maana zikimaliza katika nafasi mbili za juu za ligi hiyo.

Mabosi wa Simba walikubaliana kuvunja mkataba na Jobe waliyemsajili katika dirisha dogo la ligi iliyokwisha kutokana na kutoridhishwa na kiwango alichokionyesha, lakini kwake imekuwa kama zali kwani fasta ameibukia Nouadhibou iliyoishia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kimeliambia Mwanaspoti, kuwa mchezaji huyo wakati anasubiri kuvunjiwa mkataba tayari alikuwa na ofa nyingi mezani.

“Jobe atashiriki Ligi ya Mabingwa msimu huu hii ni baada ya kumalizana na Nouadhibou FC ambao ni mabingwa wa ligi na tayari wamefuzu kushiriki michuano hiyo hivyo licha ya kuachwa na Simba bado ana nafasi kubwa ya kuonekana kimataifa na huenda akawa na msimu mzuri huko,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;

“Baada ya Jobe kufanya mazungumzo na Simba ya kutaka kumtoa kwa mkopo alikataa kwani alikuwa tayari amepata ofa nzuri hivyo aliuomba uongozi wamalizane naye kwa kumvunjia mkataba ili aweze kusajiliwa akiwa mchezaji huru hilo limefanyika na msimu ujao atacheza huko.”

Alipotafutwa Jobe mwenyewe ili kuzungumzia dili hilo alisema kwasasa ni mchezaji huru kuhusiana na kusajiliwa na timu nyingine sio suala ambalo litashindikana huku akikiri muda ukifika kila kitu kitawekwa wazi.

“Nimemalizana na Simba na nashukuru kwa miezi sita niliyocheza huko, sitaki kuzungumza mengi kuhusiana na kuondoka kwa vile nimeondoka vizuri na kila nilichokuwa nakitaka nimepewa naamini kuhusishwa na timu ni muda sahihi na nikimalizana nayo kila mmoja atafahamu ukweli ulivyo,” alisema Jobe na kuongeza;

“Mpira ndio kazi yangu na kuondoka kwangu Simba sio mwisho wangu, nafikiri msimu ujao nitacheza, kuhusu timu ni suala la muda tu lakini mtarajie kuniona na naamini nina mashabiki Tanzania ambao wataendelea kunifuatilia nawapenda sana wote.”

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: