Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ivory Coast paka mwenye roho saba

Ivory Coast Yaifurusha Senegal AFCON Ivory Coast paka mwenye roho saba

Tue, 6 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mafanikio ya Ivory Coast kufika nusu fainali baada ya kuanza vibaya hatua ya makundi ikiwamo kula kipigo cha kudhalilishwa hadi kumfukuza kocha, yamefananishwa na stori ya paka mwenye roho saba.

Kocha wa mpito wa Emerse Fae ameielezea safari ya timu hiyo kutoka kuwa ‘unga’ kabisa hadi kutinga kibabe nusu fainali kuwa ni kisa cha “kufa na baadaye kufufuka.”

Wenyeji walishinda mechi moja tu ya hatua ya makundi, iliyokuwa ya ufunguzi dhidi ya Guinea Bissau na kisha ikaja kuchapwa 1-0 na Nigeria kabla ya kudhalilishwa kwa kipigo cha kwanza kikubwa zaidi katika historia yao cha 4-0 kutoka kwa Equatorial Guinea, jambo lililolifanya Shirikisho la Soka la Ivory Coast kumtimua kocha Jean-Louis Gasset na kumteua Emerse Fae kama kocha wa mpito.

Hata hivyo, Ivory Coast ilitinga hatua ya mtoano ya 16-Bora ikipenya kupitia tundu la sindano ikiwa moja ya timu nne zilizofuzu kama ‘best loosers’.

Walikuja kuibuka kibabe na kuwatoa mabingwa watetezi Senegal kwa penalti, lakini mechi ya kupindua meza kishujaa zaidi ilikuwa ni dhidi ya Mali katika robo fainali.

Mali walitawala mchezo na kupata bao la kuongoza kisha kabla ya mapumziko nahodha na beki wa kati wa wenyeji Idilon Kossounou akatolewa kwa kadi nyekundu.

Lakini wakati wengi wakionekana kutarajia ushindi kwa Mali huku mpira ukiingia katika dakika ya 90, kinda mtokea benchini, Simon Adingra akaweka bonge la bao la kusawazisha na kuipeleka mechi katika dakika 30 za ziada. Na katika dakika ya 120+2 Ouamar Diakite akafunga la ushindi kwa kisigino akisindikiza shuti la Seko Fofana na kuipeleka Ivory Coast nusu fainali ikiwa na watu tisa uwanjani.

“Niliwaambia wachezaji kwamba tulikuwa tumekufa baada ya kipigo cha Equatorial Guinea, na tukafufuka baada ya mechi ya Morocco dhidi ya Zambia,” Fae alisema.

“Nilikuwa na hisia kali sana zikipita kichwani mwangu, nikijaribu kuchakata hali halisi iliyotokea. Unapofika nusu fainali, unacheza na timu zenye ubora wa juu zaidi, hivyo tutajiandaa vyema,” Fae aliongeza.

Mabingwa mara mbili wa Afcon, Ivory Coast sasa wataivaa DR Congo katika nusu fainali kesho huku pia wakichungulia nusu fainali ya Afrika Kusini vs Nigeria kumjua wa kwenda fainali.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: