Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hofu ya dakika 10 Euro 2024

Vargassss Hofu ya dakika 10 Euro 2024

Tue, 25 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kichapo cha Scotland kwenye Euro 2024 mbele ya Hungary kiligubikwa kwa hofu ya zaidi ya dakika 10 baada ya mchezaji Barnabas Varga kuumia vibaya kwenye mchezo huo.

Straika huyo wa Hungary, Varga, 29, aligongana na kipa wa Scotland, Angus Gunn akikutana na kiwiko kilichomuumiza vibaya usoni.

Varga alianguka chini na kupoteza fahamu jambo lililofanya mwamuzi kusimamisha mchezo haraka ili mchezaji huyo kupata nafasi ya kutibiwa.

Wachezaji wenzake waliwahi haraka kumsaidia Varga kuwa kwenye hali nzuri.

Madaktari walilazimika kuingia uwanjani haraka kumsaidia mchezaji huyo na hivyo kulazimika kuzungushiwa uzio na wachezaji wenzake ili kuweka hali ya usiri wakati alipokuwa akifanyiwa matibabu.

Wachezaji kadhaa walionekana wenye fadhaa, akiwamo staa wa Liverpool na nahodha wa Hungary, Dominik Szoboszlai, aliyeonekana akimwaga machozi.

Wakati Varga akionekana kwenye hali ya kutojifahamu, Szoboszlai alikimbia hadi nje ya uwanja kuchukua machela kwa ajili ya kumbeba mchezaji huyo kumwahisha hospitalini. Baada ya dakika 10, Varga alibebwa kutoka uwanjani na kufanya mashabiki kupiga makofi uwanja mzima.

Baadaye staa huyo alipandishwa kwenye gari la wagonjwa na kupelekwa hospitalini, huku matumaini yaliyoibuka ilikuwa mchezaji huyo kurudi kwenye fahamu na kuwasiliana.

Kocha wa Hungary, Marco Rossi alisema mchezaji Varga atafanyiwa upasuaji baada ya kuumia mifupa ya uso. Straika huyo anayechezea klabu ya Ferencvaros hatacheza tena kwenye fainali za Euro 2024.

Rossi alisema: "Maisha ya Barnabas Varga hayapo tena kwenye hatari. Atafanyiwa upasuaji baada ya kuumia sana usoni na hatakuwapo kwenye mechi zilizobaki za Euro 2024."

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: