Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa mastaa wasepe, wabaki Simba

Simba Squad Warm Up.jpeg Hawa mastaa wasepe, wabaki Simba

Tue, 28 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba inapita kwenye kipindi kigumu, ambacho hakikutegemewa kwa siku za hivi karibuni kutokana na mafanikio ya nyuma.

Ni timu ambayo hadi sasa msimu huu imepoteza mchezo mmoja tu, ilipochapwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga, lakini inavyozungumzwa nje ni kama imeshapoteza michezo saba kati ya minane ambayo imecheza.

Ni wachache sana nje ya Simba ambao wanalaumu kuhusu kiwango, huwezi kumuona shabiki wa Yanga akizomea kuhusu kiwango cha Simba, lakini utawaona Simba wenyewe wakilalamika kuhusu timu yao. Ukibaki kwenye uhalisia kuna sehemu kuna tatizo lakini siyo kwa kiwango kikubwa hivyo.

Msimu uliopita Simba ilitolewa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini ilipigwa mawe kuliko timu nyingine yoyote ile, ilishika nafasi ya pili kwenye ligi, ikaonekana haijafanya jambo lolote.

Shida ya Simba msimu huu, ilianza tangu kwenye usajili baada ya mashabiki kuaminishwa kuwa timu hiyo imesajili mastaa wakubwa ambao wanaweza kuifikisha hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini baada ya kuingia uwanjani, kiwango cha wageni zaidi ya wanane kati ya 10 kimefeli na kuanza kuzua maswali mengi.

Bahati mbaya Simba wanashindana na Yanga, lakini kuna hofu kama Yanga wanashindana na Simba, kwa kuwa Yanga ikipoteza mashabiki wake wanakuwa wapole, Simba ikipoteza mashabiki wake wanakuwa wakali, ikitoa sare wanawaka haswa, ikishinda bado wanalaumu kiwango, hili ni daraja walilojiwekea.

Hata hivyo, kutokana na hali ilivyo kwa sasa Simba hawaepuki kupiga panga kwenye kikosi chao, ili mambo yakae sawa ni lazima wakubali kuanza upya, kuna wachezaji wanaweza kubaki kulingana na viwango vyao, lakini wengine wanatakiwa kuondoka.

Kuna mambo mawili, Simba wanatakiwa kuwa makini na usajili wa Januari kwa kuwa mara nyingi ni wachezaji wachache wanapatikana sokoni na wengi ni wale ambao kwenye timu zao wameonekana hawana kiwango sahihi, hivyo pamoja na ukweli kwamba wanatakiwa kupiga panga ili kupata kikosi bora, bado kuna wengine watalazimika kusubiri hadi Julai kwenye dirisha kubwa.

Ni ukweli kwamba wachezaji wachache tu ndiyo wanaonekana kuwa wanaweza kubaki Simba wakawa na msaada kwa timu hiyo ingawa wengine watabaki na kukaa benchi, kama timu hiyo itakuwa na msuli mkubwa wa kufanya usajili kabambe;

WABAKI:

Aishi Manula

Hakuna swali kuwa Manula ni kati ya makipa bora, mafanikio makubwa ya Simba kwenye msimu minne nyuma yameanzia kwake.

Kinachomsumbua kwa sasa ni majeraha na siyo kiwango sahihi uwanjani.

Kitendo cha kuwa uwanjani halafu Simba wakalala kwa mabao 5-1 dhidi ya Yanga, wanatakiwa kulaumiwa makocha wa timu hiyo zaidi kuliko Manula kwa kuwa ndiyo alikuwa amerejea kutoka kwenye majeraha, hakuwa tayari kuanza kwenye mchezo huu mkubwa, tayari ana makombe matano ya Ligi Kuu Bara, Robo Fainali Ligi ya Mabingwa mara tatu na Shrikisho Afrika mara moja.

Ally Salim (akae benchi)

Ni kipa kijana wa Simba, amefanya kazi kubwa kulingana na umri wake na uzoefu alionao. Alikaa langoni na kuipa Simba Ngao ya Jamii mbele ya Yanga, lakini akionyesha uwezo wa juu kwenye mchezo huo baada ya kuokoa mikwaju mitatu.

Hastahili kuwa kipa namba moja wa Simba, ila anaweza kubaki kuendelea kupata uzoefu nyuma ya Manula na Ayoub Lakred.

Ayoub Lakred

Ni kipa mwenye uzoefu wa kutosha kucheza timu kubwa kama Simba, akiwa alishatumika timu kubwa za FAR Rabat ya Morocco na RS Berkane sasa ana miaka 28 ukiwa ndiyo umri sahihi kwa makipa.

Amefika Simba wakati ambao kila mmoja hafanyi vizuri ndiyo maana anapita kwenye upepo huo, lakini kiwango chake kwenye mchezo dhidi ya Asec kinadhihirisha ubora wake, huyu anatakiwa kubaki na kuwania nafasi na Manula.

Shomary Kapombe/ Mohammed Hussein (wakae benchi)

Wanapigwa vita na baadhi ya mashabiki wa Simba, lakini kiuhalisia bado kila kocha anayetua Simba amekuwa akiwaamini kwenye namba ni wachezaji wazuri hadi sasa hawana makosa makubwa, ili kutokana na kutumika wenyewe kwa muda mrefu wanaonekana kuchoka haraka, Simba wanaweza kubaki nao kwani hadi sasa namba zao zinawabeba wakiwa ni mabeki wenye asisti mbilimbili kwenye ligi, lakini wakasajili wachezaji wengine kwenye nafasi zao wenye uwezo wa juu zaidi yao hawa wakawa wachezaji wa akiba kama wakizidiwa uwezo.

Mzamiru Yassin

Ni kiungo panga pangua Simba kutokana na uwezo wake, amekuwa kwenye ubora wa juu msimu wa pili sasa akiitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa mfululizo kwa wazawa ni ngumu kupata mchezaji mwenye uzoefu kama Mzamiru, kwa sasa akiwa amebadilika kwa kiwango cha juu kwenye uwezo wa pasi na kukaba, anastahili kubaki.

Sadio Kanoute/ Fabrice Ngoma

Kombinesheni yake na Fabrice Ngoma imeonekana kuzaa matunda kwenye michezo mingi, wameonekana kuwa bora na kuwa kati ya wachezaji bora wa kimataifa kwenye timu hiyo.

Kanoute msimu uliopita alifanya vizuri, msimu huu ameanza kwa kasi ya chini na kukosa michezo kadhaa ya mwanzoni, lakini ubora wake umeendelea kuonekana baada ya kucheza pamoja na Ngoma kwenye michezo mingi msimu huu.

Umri wake raia huyu wa Mali bado ni mdogo, ni ngumu kumkuta kwenye sababu binafsi za timu kupoteza mchezo.

Kwa upande wa Ngoma ni kati ya wachezaji walioingia kwenye dirisha kubwa la usajili na hadi sasa ameshacheza kwenye michezo yote mikubwa ya timu hiyo, usajili wake unatajwa kuwa bora zaidi msimu huu, hawa wanatakiwa kubaki.

Moses Phiri/ Che Malone Fondoh

Phiri amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba kwa kipindi kirefu, wengi wamekuwa wakiamini kuwa ni mchezaji anayetakiwa kupata nafasi tofauti na jinsi anavyopata, msimu uliopita alifunga zaidi ya mabao kumi pamoja na kwamba alipata muda mchache uwanjani, msimu huu pia hajapata nafasi ya kutosha lakini hadi sasa tayari ana mabao matatu yote akiwa amefunga akiwa ndani ya eneo la 18 la timu pinzani.

Malone ndiye kipenzi kwa mashabiki wa Simba kwenye eneo la ulinzi akiwa ameanza na kasi mwanzoni mwa msimu akitokea Cotton Sport ya nchini kwao Cameroon, ametumika kwenye michezo yote muhimu ya Simba na hakuna mchezo alioonyesha kiwango cha chini tangu amejiunga nao mwanzoni mwa msimu, huyu anatakiwa kubaki kwenye timu hiyo.

Luis Misquissone (benchi)

Bado Luis hajawaridhisha mashabiki wa Simba kwa kuwa walifikiri mambo makubwa zaidi kutoka kwake, lakini kiwango chake na muda anaopata bado kinaridhisha akiwa hadi sasa ana asisti tatu kwenye michezo nane ya ligi.

Hiki ni kiwango kizuri kwa upande wa namba, ikiwa inaonekana kuwa anaweza kufanya vizuri zaidi akipata nafasi zaidi hadi mwishoni mwa msimu, lakini kwa sasa anaweza kukaa benchi wakati Simba wanajitafuta.

Jean Baleke/ Kibu Denis

Labda Baleke ndiye mchezaji bora zaidi kwa Simba hadi sasa... akiwa ameshafunga mabao saba kwenye Ligi Kuu akiwa kinara, na amekuwa na uwezo mkubwa kwenye michuano ya kimataifa, ni sahihi kubaki kwenye timu hiyo kwa sasa kwa kuwa anaweza kuwapitisha kwenye wakati wowote mgumu. Kibu alijiunga na Simba akionekana kuwa mchezaji wa kawaida lakini kocha Olivier Robert Robertinho alimbadilisha na kumfanya kuwa mahiri, pamoja na kwamba msimu uliopita alifunga mabao mawili tu, lakini kasi uwezo wa kukaba na kushambulia ambao amekuwa akiuonyesha unawaridhisha mashabiki wa timu hiyo msimu huu akiwa ameifungia timu yake bao pekee kwenye mchezo waliopoteza 5-1 na Yanga, anaweza kuwa staa wa timu miaka kadhaa ijayo.

Clatous Chama(akae benchi)

Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu uwezo wa Chama, labda ni kwa kuwa amekuwa akionyesha uwezo mkubwa wakati mwingine na wakati mwingine anashuka, huku kwenye namba huwezi kumuacha akaondoka Simba.

Chama hadi sasa ana mabao mawili kwenye nafasi yake ni kati ya wachezaji waliofanya vizuri, anaweza kuwa ameshuka kiwango lakini Simba inatakiwa kubaki naye na kusajili mchezaji mwingine mwenye uwezo zaidi yake ambaye anaweza kumweka benchi.

Inonga Bacca

Inonga hakuna ubishi ni beki bora ambaye amedhiirisha uwezo wake kwa msimu wa tatu sasa na kuitwa timu ya Taifa ya DR Congo ni ngumu kufikiri kuhusu kuachana naye, amakuwa mhimili muhimu kwenye kila mchezo.

Kennedy Juma/ Israel Mwenda

Kwa wachezaji wa ndani hawa ni kati ya wale bora kwenye nafasi zao za ulinzi.

Kennedy amekuwa akipambana kwa muda mrefu kuhakikisha anakuwa na nafasi ya kudumu kwenye timu hiyo, lakini shida kubwa imekuwa uwepo wa Inonga na Malone, anaonekana kuwa mmoja kati ya wale ambao wanaweza kuwa nyuma ya mastaa hao wa kigeni lakini akiwa pia na uzoefu wa kutosha.

Kwa upande wa Mwenda amekuwa hapati nafasi mara kwa mara lakini kila anapocheza anaonyesha uwezo mzuri, kwa kuwa ni mzawa anaweza kuendelea kubaki kwenye timu hiyo au aende kwa mkopo.

Hussein Hasan/ Ismail Abdallah/ Ahmed Farouz

Hawa walipandishwa kutoka kwenye timu ya vijana, bado wanatakiwa kuewa muda wa kutosha kuendelea kupata uzoefu kwenye timu, wasiharakishwe.

WASEPE

Iddi Chilunda

Ulikuwa usajili wa mshangao kwa wengi, hakuwa anapewa nafasi ya kutua kwenye timu hiyo, hajapata nafasi kutokana na uwezo mazoezini na hata mchezo mmoja aliocheza dhidi ya Namungo hakuonyesha kiwango kizuri, Simba wanaweza kuachana naye.

Nasoro Kapama

Alitajwa kama kiraka kwenye timu hiyo, lakini kwenye zaidi ya michezo 17 ambayo Simba imecheza msimu huu hajapata nafasi, ni wakati wake wa kuondoka na kuwaachia wengine nafasi.

Aubin Kramo

Huyu ni kati ya wachezaji waliosajiliwa wakipewa jina kubwa sana, alitoka Asec sehemu ambayo alitoka Yao Kouassi, Pacome Zouzou na Aziz Ki ambao wanafanya vizuri wakiwa na Yanga.

Shida yake siyo kiwango bali majeraha ya muda mrefu yamenyima nafasi ya kucheza, kwenye soka hakuna nafasi ya kusubiri, ni vyema Simba wakaachana naye na nafasi yake asajiliwe mchezaji mwingine.

Hussein Bakari ‘Kazi’,

Kazi msimu uliopita alionyesha kiwango cha hali ya akiwa na Geita na alitarajiwa kuwa anaweza kutoa upinzani kwa Malone na Inonga, lakini mambo yamekuwa magumu kwake akiwa hajapata nafasi ya kutumika uwanjani, ni sahihi kuwa anaweza kupewa mkono wa kwaheri wasajiliwe wanaoweza kucheza.

Jimson Mwanuke

Aliponea chupuchupu kwenye usajili uliopita, bado hajaonyesha chochote kwenye timu hiyo hadi sasa, anaweza kuondoka kwenda kucheza sehemu nyingine.

John Raphael Bocco

Huyu ndiye mchezaji mzoefu zaidi kwenye kikosi cha Simba, akipata nafasi kwenye dakika 20 za mwisho anaonyesha kitu lakini ni muda sasa wa kuondoka na kuwaacha vijana waonyesha makali yao,anaweza kuwa meneja au kocha wa vijana.

David Kameta/ Husein Abel

David Kameta Duchu alirejea Simba akitajwa kuwa anakwenda kupata nafasi moja kwa moja, lakini mambo yamekuwa magumu kwake, hajapata nafasi yoyote na amekuwa akiishia jukwaani au kwenye benchi, kama ilivyo kwa kipa Hussein Abel ambaye alielezwa kuwa anakwenda kupata nafasi mbele ya Aishi Manula.

Hawa ni wachezaji wa ndani ambao bado wana timu nyingi ambazo wanaweza kucheza, wanaweza kuondoka kwa sasa na kutafuta nafasi sehemu ambazo watapata nafasi.

Saido Mtibazonkiza

Saido msimu uliopita alikuwa mfungaji bora akiwa na mabao 17 sawa na Fiston Mayele, mwanzo wa msimu huu siyo mbaya kwake, akiwa ana bao moja la penalti kwenye Ligi Kuu Bara sawa na Ligi ya Mabingwa Afrika, siyo takwimu mbaya kwake, anaweza akiwa ni mchezaji mwenye uzoefu wa hali ya juu, Simba wanaweza kuachana naye na kutafuta mchezaji mwingine.

Willy Onana

Hajaonyesha ubora wake pamoja na kupata nafasi mara kwa mara, uwezo wake na kasi vimeonekana kuwa vitu viwili tofauti, alianza kutabiriwa mabaya kutokana na ligi aliyotoka ya Rwanda, haonekani kama ni mchezaji anayeweza kubaki Simba akafanya vizuri.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: