Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fadlu apania kuweka rekodi CAF

Simba Vs Fadlu Fadlu Davids.

Tue, 20 Aug 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amewaambia wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuwa wawe na subira kidogo, kwani kikosi chake kinaelekea kwenye ubora anaouhitaji, na ana uhakika itakuwa ni tishio zaidi si hapa nchini tu bali Afrika.

Raia huyo wa Afrika Kusini alitoa kauli hiyo juzi, baada ya kumalizika kwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hiyo na Tabora Uited, ikishinda mabao 3-0, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.

Kocha huyo alisema bado anaendelea na kazi yake ya kukiimarisha kikosi hicho, lakini akiridhika na jinsi walivyocheza na kupata ushindi huo.

"Timu inaanza kuimarika, siku hadi siku inaelekea kwenye ubora ninaotarajia, mashabiki wa Simba wawe na subira kwa sababu bado tunaendelea kukiweka kikosi kwenye hali nzuri, na kukifanya kiwe bora zaidi na tishio.

Bado tuna shughuli ya kufanya, ukiangalia katika mechi hii ilikuwa tuiue mapema tu kipindi cha kwanza na kipindi cha pili tucheze bila presha kwa kuudhibiti na kuumiliki mchezo, lakini haikuwa hivyo, tukalazimika kusaka mabao ya kuumaliza mchezo kipindi cha pili, lakini nimeridhika, ila nimehuzunika kuumia kwa Mutale (Joshua), kidogo kidogo tunakwenda," alisema Fadlu ambaye ndiyo msimu wake wa kwanza kuifundisha timu hiyo akitokea, Raja Casablanca ya Morocco.

Yalikuwa ni mabao ya beki wa kati, Fondoh Che Malone, Valentine Mashaka na Awesu Awesu, yaliyofanya Simba kupata ushindi wa mabao 3-0, yaliyoipeleka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.

Francis Kimanzi, Kocha Mkuu wa Tabora United, alisema hawezi kuwalaumu wachezaji wake kwa sababu wamekutana na mechi kubwa na ngumu, dhidi ya timu imara

"Nafikiri wapinzani wetu walikuwa bora, wamefanya kile walichotaka kufanya, wana vitendea kazi bora kuliko sisi kwa maana ya wachezaji, sitaki kuwaangusha wachezaji wangu kwa sababu wamefanya vema, wamefanya kila walichokiweza, ndiyo maana siko hapa kuzungumzia jinsi tulivyofungwa, tunatengeneza timu taratibu baadaye tutakuwa timu bora," alisema raia huyo wa Kenya.

Wakati Tabora United itakwenda mkoani Lindi kucheza dhidi ya Namungo, Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Jumapili ijayo, siku hiyo hiyo, Simba itakuwa nyumbani, Uwanja wa KMC, Mwenge, ikiikaribisha, Fountain Gate.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: