Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fadlu aikubali Simba mpya

Simba Sc Usajili Wachezaji wa Simba mazoezini nchini Misri.

Mon, 15 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Klabu ya Simba ikisema haijamaliza kufanya usajili wake kuelekea msimu ujao, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fadluraghman Davids 'Fadlu', amesema anataka kutengeneza kikosi cha wachezaji wenye kiu, njaa ya ushindi na mafanikio, huku msingi wake ukiwa ni ushambuliaji zaidi.

Akizungumza wakati akiwa Ismailia nchini Misri ambako kikosi hicho kimeweka kambi kujiandaa na msimu ujao wa mashindano, kocha huyo raia wa Afrika Kusini, ambaye amepewa jukumu la kukinoa, akiwa mpya, na wachezaji wengi wapya, amesema pamoja na kuwafundisha mifumo ya uchezaji na staili mbalimbali, lakini anataka kuwajenga wachezaji wake wawe watu wa kupambana kusaka ushindi kwa nguvu na hali yoyote wanapokuwa uwanjani.

"Timu hii ina mashabiki wengi sana, kwa hiyo haiwezekani wachezaji wawe wanacheza tu kama kujifurahisha, nataka wawe wanacheza kwa malengo, wakipambana, wakitumia mafunzo tunayowapa wakichanganya na vipaji vyao kwa ajili ya kupambania nembo ya klabu na kuwajali mashabiki wao waliowafuata. Na hakuna kingine bali ni kucheza kwa kushambulia kwa kasi na kusaka ushindi, hili ni lazima likae kichwani mwa wachezaji wangu," alisema kocha huyo maarufu kwa jina la Fadlu.

Tayari kocha huyo alishabainisha kuwa anataka kutengeneza safu moja kali ya ushambuliaji ambayo itakuwa inafunga mabao mengi ili kushinda mchezo wa mpira wa miguu, kwani alisema usipofunga, basi ni lazima utatoka sare au kufungwa.

Alisema ili kufanya hivyo ni lazima atengeneze muunganiko, maelewano, mikimbio ya kusaka nafasi, mawasiliano ya mdomo na mwili kwa mastraika wake ili wafunge mabao mengi kama alivyokuwa anafanya yeye enzi zake, ambapo ameshawahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu nchini Afrika Kusini mara mbili kwa nyakato tofauti wakati akicheza soka.

Wakati Simba ikiendelea kujifua nchini Misri jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Crescentius Magori, amesema bado hawajamaliza usajili kama inavyofikiriwa.

Alisema bado wanaendelea na usajili ambao kwa mujibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), dirisha hilo linarajiwa kufungwa Agosti 15, mwaka huu.

"Bado, bado kabisa, usajili kwetu unaendelea, hatujamaliza," alisema Magori. Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa, timu hiyo ipo kwenye mazungumzo na mchezaji Jonathan Alukwu kutoka Sporting Lagos ya Nigeria.

Mchezaji huyo anayecheza winga ya kushoto na wakati mwingine kiungo mshambuliaji, yupo karibuni kujiunga na kikosi hicho ili kuimarisha upande huo, baada ya upande wa kulia kumpata Jushua Mutale kutoka Power Dynamos ya Zambia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: