Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Fadlu abaini tatizo Simba

FADLU SIMBA Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

Tue, 30 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kukiongoza kikosi chake kuibuka na ushindi wa pili mfululizo katika mechi za kirafiki kujianda na msimu mpya nchini Misri, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, ameeleza kufurahishwa na namna wachezaji wake wanavyojituma uwanjani na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini bado kuna tatizo anapaswa kukabiliana nalo.

Juzi Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Telecom Egypt FC, ikiwa ni mwendelezo wao wa ushindi kwenye mechi za kirafiki baada ya ile ya kwanza dhidi ya  El-Qanah kushinda 3-0.

Akizungumza baada ya mechi, hiyo ya juzi, Fadlu alisema kama mastraika wake wangekuwa makini, basi wangetoka na ushindi wa mabao 7-1 katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Mercure.

Alisema wachezaji wake walicheza kwa kiwango bora wakitengeneza nafasi nyingi, lakini kilichomsikitisha ni upande wa mastraika kukosa mabao mengi ya wazi, kitu ambacho alidai anahitaji kukifanyia kazi kabla ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Afrika kuanza.

"Katika mechi hii tulikuwa tufunge mabao sita hadi saba kwa sababu tulitengeneza nafasi nyingi sana, kinachonishangaza zinashindwa kutumiwa vizuri, wakati wenzetu wamepata nafasi moja tu ya kupiga langoni na wamefunga, lakini kizuri hapa ni kuwa tunatengeneza nafasi za kufunga.

"Kinachotakiwa ni wachezaji kukimbia kwa wakati, mmoja anapokuwa pembeni basi kuwe na namba nyingi ndani ya lango na kumalizia kwa usahihi," alisema kocha huyo raia wa Afrika Kusini, ambaye ameanza kukinoa kikosi hicho msimu huu akitokea Wydad Casablanca ya Morocco.

Hata hivyo, alisema timu imeimarika wachezaji wanaonyesha ushindani baina yao kwa wao katika kuwania namba kwenye kikosi cha kwanza.

"Nafurahia namna wachezaji wanavyojituma na kubeba majukumu kwa kila anayepata nafasi, michezo miwili ya kirafiki tuliyocheza imetupa mwanga wa kufikia malengo yetu na kile ambacho tunakitaka," alisema Fadlu.

Aliongeza; "Tutakuwa na mchezo mwingine wa kirafiki Dar es Salaam kwenye Simba Day..., michezo hii ya kirafiki ni muhimu sana, kipo kitu tulichokitengeneza kwenye kambi yetu ambacho mashabiki watakiona."

Kocha huyo amebainisha kuwa kikosi hicho kinatarajia kuanza safari ya kurejea nchini kesho jioni kwa ajili ya maandalizi ya tamasha la Simba Day. "Nafikiri tuko mwishoni mwa 'pre season' yetu, tutaanza kurejea Jumanne jioni, tumefanyia mazoezi vitu vingi, ufundi, mbinu, kasi na utimamu wa mwili," alisema.

Ikiwa nyuma kwa bao moja katika mechi hiyo ya juzi, Simba ilipindua meza kwa kufunga mabao mawili kipindi cha pili, yaliyofungwa na Mashaka Valentino aliyesajiliwa msimu huu akitokea Geita Gold na Ladack Chasambi.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Valentino aliyefunga bao la kusawazisha akiunganisha mpira wa krosi kutoka kwa beki mpya wa kushoto raia wa Burkina Faso, aliyesajiliwa kutoka FC Saint Lupopo ya DR Congo,Valentine Nouma, alisema maelekezo ya kocha ndiyo yaliyomfanya kupachika bao.

"Mchezo ulikuwa mgumu, mwalimu alikuwa anataka tushambulie muda wote na wakati naingia kipindi cha pili alichoniambia ni kukaa eneo sahihi kwenye lango, aliniambia unaweza ukakosa, lakini baadaye nitafunga na kweli ikawa hivyo," alisema.

Kwa upande wake, Chasambi aliyepachika bao baada ya pasi maridadi kutoka kwa beki wa kulia, Kelvin Kijili, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Singida Big Stars, alisema lilikuwa ni moja kati ya bao bora kuwahi kufunga.

Simba ilitarajiwa kucheza mechi yake ya mwisho jana usiku kwenye Uwanja wa New Suez Canal, dhidi ya Al-Adalah FC inayocheza Ligi Daraja la Kwanza ya nchini Saudi Arabia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: