Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

England yajiweka njia panda Euro 2024

England Attack England yajiweka njia panda Euro 2024

Tue, 25 Jun 2024 Chanzo: Mwanaspoti

England haina namna nyingine zaidi ya kuichapa tu Slovenia leo Jumanne ili kumaliza vinara kwenye Kundi C.

Kuna sababu ya kufanya hivyo. Kama itashindwa kumaliza kinara kwenye kundi lake katika fainali hizo za Euro 2024, basi safari yao ya kwenda kutimiza ndoto za kunyakua taji hilo itakuwa ngumu kwelikweli.

Isipomaliza kinara kwenye kundi lake, kikosi hicho cha Three Lions kinachonolewa na kocha Gareth Southgate kitalazimika kupita kwenye njia ngumu katika kuelekea fainali ya mikikimikiki hiyo inayofanyika huko Ujerumani.

England ilicheza kwa kiwango cha hovyo sana katika mechi ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Denmark na hivyo kuamsha wasiwasi mkubwa kwa mashabiki wa timu hiyo, wakiamini timu hiyo huenda isimalize vinara kwenye kundi lao.

Na kama England itashindwa kupata ushindi dhidi ya Slovenia hiyo ina maana watalazimika kucheza na vinara wa Kundi A kwenye mchezo wa Raundi ya 16 bora, ambao ni wenyeji Ujerumani.

Ujerumani ilitoka sare ya bao 1-1 na Uswisi kwenye mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi uliofanyika usiku wa Jumapili, hivyo inasubiri tu kumenyana na timu itakayomaliza nafasi ya pili kwenye Kundi C katika hatua inayofuata na hicho ndicho ambacho England itapambana kukikwepa.

England inataka kumaliza kinara kwenye kundi lake, ili kucheza na timu itakayokuwa imeshika nafasi ya pili kwenye Kundi A, ambao kwa sasa ni Uswisi ya mkali Xherdan Shaqiri.

Endapo England itamaliza nafasi ya pili kwenye Kundi C, itacheza na Ujerumani kwenye hatua ya 16 bora na ikishinda hapo, itakipiga na ama Hispania au timu itakayokuwa imemaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi A, D, E au F kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali.

Na kama itafanikiwa kupenya kwenye mtego huyo, basi kwenye hatua ya nusu fainali, itakipiga na ama Ureno au Uholanzi.

Endapo kote huko itakuwa imepita kwenye harakati zao za kwenda kunasa taji la Ulaya, ambalo wamekuwa wakilifukuzia kwa miaka mingi bila ya mafanikio, basi kwenye mechi ya fainali, itakayopigwa Berlin, timu ambayo inaweza kukabiliana nayo ni Ufaransa au Ubelgiji. Njia ni ngumu kwelikweli.

Lakini, kama England itamaliza nafasi ya tatu kwenye kundi lake, nini kitatokea?

Hesabu zinavyosoma, inawezekana kabisa England kumaliza nafasi ya tatu kwenye kundi. Hiyo ni kama itakubali kuchapwa na Slovenia na kisha Denmark ikaichapa Serbia, hapo Southgate na kikosi chake cha Three Lions kitaporomoka na kumaliza hatua ya makundi kwenye nafasi ya tatu.

Na matumaini yao ya kusonga mbele ikitokea hivyo, wanaamini watakuwa moja ya timu nne ambazo zitavuka kwenye hatua ya makundi na kuingia mtoano wa 16 bora kama timu ya tatu bora kwenye hatua ya makundi.

Kwa kuzingatia hilo na namna watakavyopangwa kwenye hiyo nafasi ya mshindi wa tatu bora kwenye kundi, basi timu ambayo inaweza kukutana nayo kwenye hatua ya 16 bora, wanaweza kuwa vinara wa Kundi F, ambao kwa sasa ni Ureno ya supastaa Cristiano Ronaldo.

La, itakwenda kukabiliana na vinara wa Kundi E, ambapo inaweza kuwa Ubelgiji ya Kevin De Bruyne, Slovakia, Romania au Ukraine.

Ikipenya hapo, kwenye robo fainali, balaa linaweza kuwakuta kwa kumenyana na Ufaransa au Uholanzi, inategemea na timu gani itakuwa imemaliza vinara kwenye Kundi D. Na hapo kama itafanikiwa kushinda na kutinga nusu fainali, England itarudi kucheza na moja ya timu ilizokuwa imepangwa nazo kwenye Kundi C, ambapo inaweza kuwa Slovakia au Denmark au watakipiga na Italia, ambapo itakuwa marudio ya fainali Euro 2020.

Na kama Southgate na chama lake litaibuka na ushindi kwenye mechi zote hizo na kufika fainali, basi inaweza kwenda kukipiga na ama Hispania au Ujerumani kwenye kipute hicho cha mwisho kabisa kwenye Euro 2024.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: