Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama jana, leo na kesho, magwiji wamzungumzia

Realclatouschama Kiungo wa Simba, Clatous Chama

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba juzi ilionyesha ukubwa wake kwa kushinda ugenini ikiichapa Tabora United mabao 4-0, huku staa wake Clatous Chama aliyekuwa amesimamishwa kwa makosa ya kinidhamu akirejea na kuonyesha tofauti yake na wachezaji wengine kikosini hapo.

Chama alisimamishwa Desemba 11, mwaka jana sambamba na Nassoro Kapama lakini alisamehewa Januari 29 na kujiunga na timu mkoani Kigoma na kuanza kucheza kwenye mechi dhidi ya Mashujaa Februari 3 mwaka huu alipoingia dakika ya 71 akichukua nafasi ya Mzamiru Yassin na kucheza kwa ubora na kuifanya Simba kishinda 1-0.

Kiungo huyo aliwasha moto zaidi kwenye mechi iliyofuata juzi, dhidi ya Tabora United alipocheza kwa kiwango cha juu na kuwakosha mashabiki wa Simba ambao wengi wao baada ya mechi waliweka wazi walikuwa wamemmisi mkali huyo aliyethibitisha ubora wake wa ‘jana’ ndio huohuo wa ‘leo’ na bila ya shaka ‘kesho’.

Staa huyo wa timu ya taifa ya Zambia katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, Tabora alihusika moja kwa moja kwenye mabao mawili ya timu hiyo akitoa asisti mbili; ya bao la kwanza alipopiga mpira wa frii-kiki na kumkuta Pa Omar Jobe aliyefunga kwa kichwa katika dakika ya 19 na kurudia tena dakika ya 60 akipiga mpira uliomkuta Che Malone Fondoh kwenye boksi la Tabora na kuweka mpira nyavuni.

Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Freddy Michael dakika ya 87 kwa asisti ya Luis Miquissone na Sadio Kanoute dakika 36 kwa asisti ya Shomari Kapombe.

Chama amejitengenezea ufalme wa asisti kwenye Ligi Kuu ambapo msimu wa 2020/2021 alimaliza akiwa kinara akitoa asisti 15 na kufunga mabao manane kisha kuuzwa RS Berkane ya Morocco lakini aliporejea, msimu uliopita pia alikuwa kinara wa asisti akitoa 14 na kufunga mabao manne na msimu huu amefikisha asisti tatu.

Kocha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Kenny Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema Simba ilimmisi Chama kwani ni mchezaji bora anapokuwa uwanjani.

“Chama ni mchezaji mzuri, sijawahi kuwa na shaka na kiwango chake lakini huenda makocha hawamuelewi kwenye uwanja wa mazoezi ila akiwa kwenye mechi anakuwa na faida kubwa.

“Zamani alikuwapo mchezaji alikuwa anaitwa Hussein Aman Marsha, alikuwa anacheza taratibu kama Chama ila akawa hatari zaidi akiwa na mpira. Wachezaji wa aina hiyo wapo unatakiwa kuangalia zaidi nini anafanya kwenye mechi na kumpa imani,” alisema Mwaisabula na kuongeza;

“Katika kikosi cha Simba hakuna mchezaji anayeweza kuwa kama Chama hivyo walimuhitaji na kurejea kwake ataisaidia sana timu katika mechi zake.”

Kocha wa timu za taifa za Wanawake na klabu ya JKT Queens, Esther Chaburuma alisema Simba ilikuwa inamuhitaji Chama ndiyo maana ikamsamehe.

“Kama Simba wameamua kumrudisha ina maana ana umuhimu. Kwa ubora wake uwanjani naamini atawasaidia sana kwani amekuwa akifanya mambo makubwa anapopewa nafasi,” alisema Chaburuma.

Kiungo wa zamani wa Taifa Stars na klabu mbalimbali zikiwemo Simba, Yanga na Stand United, Amri Kiemba alisema Chama ni mchezaji mzuri na kila mtu anajua hilo ila kwa sasa hawezi kuzungumzia urejeo wake kwani amecheza mechi mbili tu.

“Ubora wa Chama kila mtu anaujua. Kwenye urejeo wake nadhani tusubiri walau baada ya mechi mbili ndipo tutazungumzia ubora wake lakini akiwa fiti ni mchezaji ambaye an afaida kubwa kwenye timu,” alisema Kiemba.

Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na alama 29 baada ya michezo 12 chini ya vinara Yanga yenye pointi 34 mechi 13 na Azam pointi 31 mechi 13.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: