Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Benchikha ana siku sita

Benchikha Mapinduzi.jpeg kocha Abdelhak Benchikha

Mon, 15 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba imesharejea jijini Dar es Salaam tangu jana mchana ikitokea Singida, ilipoenda kucheza na Ihefu na kutoka sare ya 1-1, kisha mastaa wa timu hiyo wakapewa mapumziko mafupi, huku kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha akitoa kauli ya siku sita alizonazo kabla ya kukabiliana na Yanga kwa mara ya kwanza.

Yanga na Simba zinatarajiwa kuvaana katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara, pambano litakalokuwa la kwanza kwa Benchikha kwani mchezo wa kwanza uliopigwa Novemba 5 mwaka jana na Simba kupasuliwa mabao 5-1, kocha alikuwa ni Mbrazili Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyefutwa kazi na kumpisha Mualgeria huyo.

Benchikha ambaye juzi mara baada ya mchezo dhidi ya Ihefu alishtua alipoamua kubaki benchini peke yake wakati timu na mashabiki wakiwa wameshatoka kwenye Uwanja wa Liti, amelia na mastaa wa kikosi hicho kwa kushindwa kumaliza mechi kirahisi.

Katika mechi hiyo ya juzi, Simba ilisubiri hadi dakika ya 72 kupata penalti iliyowekwa kambani Clatous Chama baada ya wenyeji kutangulia kwa bao la dakika za mwishoni za kipindi cha kwanza lililowekwa kimiani na Mkenya Duke Abuya na kuifanya timu hiyo kufikisha mechi ya nne mfululizo ya mashindano matatu tofauti bila ya ushindi.

Hata hivyo, jana mara baada ya timu hiyo kuwasili jijini Dar es Salaam, Benchikha aliliambia Mwanaspoti kuwa, hatua ya kukaa peke yake haikuwa na maana mbaya zaidi ya kujipa muda wa kutafakari mambo ndani ya kikosi hicho cha Simba kilichosalia nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 20 na kukusanya pointi 46 hadi sasa.

Benchikha alisema mechi iliyopo mbele yake kwa sasa ni ngumu, lakini atajaribu kuzitumia siku sita zilizobaki kabla ya kuvaana na Yanga kubadilisha baadhi ya mambo ndani ya kikosi hicho.

Mechi hiyo ya 112 kwa timu hizo katika Ligi Kuu tangu Ligi ya Bara ilipoasisiwa mwaka 1965, itapigwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam na tayari viingilio vyake vimeshatangazwa ambapo kile cha chini kabisa ni Sh5,000, huku cha juu cha VIP A kikiwa ni Sh 50,000, VIP B Sh 30,000 na VIP C Sh 20,000 na wale watakaokaa jukwaa la Machungwa watakamuliwa Sh10,000 tu, Yanga ikiwa ndio wenyeji.

Kocha huyo raia wa Algeria akiwa hana raha usoni, alisema mafanikio ya Simba katika mchezo huo yatatoka kwenye utulivu na mabadiliko ya wachezaji wake endapo wataamua kuonyesha thamani yao.

“Hakuna ambacho kocha anaweza kufanya zaidi ya hapo tulipofika, tunatengeneza nafasi lakini tunashindwa kuzitumia inakatisha tamaa, lakini hatuwezi kusema hatutaendelea na kazi, tutajaribu kuendelea kuwapa mazoezi,” alisema Benchikha ambaye katika mechi 21 alizoiongoza Simba ameshinda 12 akitoa sare tano na kupoteza nne na kuongeza;

“Tuna siku sita kabla ya kukutana na Yanga ni mechi ngumu unapokutana na mtani wako, lakini tutaangalia kipi tunaweza kubadilisha ndani ya siku hizi ili timu ipate kile ambacho mashabiki wetu wanakitarajia. Kila kitu kinaonekana Simba inaweza kufanya kitu tofauti lakini itategemea na akili za wachezaji wataamkaje kwenye siku ya mchezo ndio maana leo (jana) tumewaambia wakapumzike ili kesho (leo) tuanze maandalizi.”

AJIFUNGIA NA VIGOGO

Jana hiyo hiyo mara baada ya Simba kurejea, kocha huyo alikuwa akisubiriwa mezani na mabosi wa Simba ambao walitaka kufanya naye kikao kizito kuhusu kikosi hicho kilichong’olewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali na ile ya Kombe la Shirikisho ikitolewa hatua ya 16 Bora na Mashujaa ya Kigoma.

Simba katika mechi hizo mbili za ugenini dhidi ya Mashujaa na Ihefu iliongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu pekee Imani Kajula, huku vigogo wakibaki mjini wakiendelea na vikao vizito kikiwemo kile cha bodi ya klabu hiyo.

Mabosi hao jana walikuwa wanakutana na Benchikha kupata maelezo yake ya kile kinachoendelea kwenye kikosi chake ikiwa ni uamuzi wa Bodi ya Simba baada ya kufanya kikao chake juzi, lakini inaelezwa ajenda kuu ni maandalizi ya mchezo huo wa Kariakoo Derby ambao Simba haitaki yawakute ya Novemba 5 ilipofyatuliwa mabao 5-1 kikiwa ni kipigo kikubwa kutoka kwa watani wao tangu mwaka 1968 ilipofungwa 5-0.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: