Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Awesu ni MVP mpya Msimbazi?

Awesu Awesu 200.jpeg Awesu Awesu

Wed, 21 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Pengine bado ni mapema sana, lakini kuna wachezaji tayari wameanza kuwasha moto mwanzoni kabisa mwa msimu.

Joshua Mutale bado anajitafuta. Steven Mukwala bado anajipiga piga kifuani. Debora Fernandez taratibu aanza kuonyesha ni kwanini Simba wamemchukua, lakini Awesu Awesu tayari gari limewaka.

Ukitazama mechi yake ya kwanza akiwa na jezi ya Mnyama Simba unaona umaridadi wa hali ya juu. Unaweza kudhani amekuwepo Simba miaka mingi.

Amecheza kama mtoto wa nyumbani. Utulivu wa hali ya juu. Ni kama mfalme wa dimba la juu amewasili.

Timu zetu hizi za Kariakoo zinahitaji mchezaji kama Awesu. Hazijawahi kuwa na muda wa kusubiri. Wao wanataka matokeo sasa. Wanataka mchezaji akiletwa leo, kesho aanze kuuwasha moto.

Awesu amekuwa na mwanzo mzuri wa maisha mapya ndani ya Msimbazi. Kama MVP angekuwa anapatikana kwa mechi moja, Awesu angekuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia siku ya kwanza Ofisini.

Alikuwa sehemu ya wachezaji waliowaweka Tabora United kwenye wakati Mgumu duru la kwanza. Pamoja na kufunga Bao kwenye mchezo huo, Awesu alioNekana kuwa mwenyeji sana eneo la mwisho la kushambulia na kama ataendelea hivyo namuona kabisa akiingia moja kwa moja kwenye Kikosi cha kwanza.

Ni aina ya mchezaji ambaye anatoa faraja kwa mashabiki anapokuwa na mali mguuni. Hana papara, boli linatembea.

Pamoja na kupata ushindi kwenye mechi dhidi ya Tabora United nadhani kuna mambo mawili bado hayajakaa sawa pale Simba.

Kwanza ni mshambuliaji na pili ni mtu wa kuchukua majukumu ya Clatous Chama kwenye eneo la ushambuliaji. Steven Mukwala ni mchezaji mzuri na kuna kila dalili kwamba ataanza kuibeba timu muda siyo mrefu, lakini kwa sasa bado anajipambania.

Ligi ndiyo kwanza imeanza, lakini kwa mshambuliaji kucheza mechi karibu nne za kirafiki bila kutupia kambani kuna namna inaanza kumsumbua.

Akifunga bao lake la kwanza ataanza taratibu kutulia. Simba imekwenda tena sokoni na kumleta Leonel Ateba. Ni mshambuliaji mwingine ambaye namba zake akiwa kwao Cameroon ukiziona ni za kibabe.

Kama akifanikiwa kuzileta kwenye soka letu, Simba watakuwa wametibu eneo la ushambuliaji. Hapo ni lazima Mnyama apate mtu wa uhakika. Eneo lingine nadhani ni pale juu namba 10.

Pale shimoni kulikompa ufalme Chama bado hapajatulia. Debora Fernandez, Joshua Mutale na Awesu ni lazima mmoja aishinde vita hii. Kuna muda kila kitu kinakwenda vizuri, lakini Simba wanamkosa mtu kama Chama pale nyuma ya washambuliaji.

Mtu flani hivi mnyumbulifu wa kulegeza viungo. Mtu flani hivi wa udambwidambwi. Huyo ndiyo bado anakosekana.

Fernandez anaonekana ni fundi wa boli, lakini bado na yeye kuna kitu hajakipata.

Yule Mukwala anaonekana ni mshambuliaji mzuri, lakini wakati mwingine hafungi ni kwa sababu ya kukosa huduma.

Wakati mwingine ni kukosa mtu anayemjulia kumchezesha. Ujio wa Awesu kuna namna utasaidia sana.

Faida kubwa anayoipata Awesu ni kuijua ligi yetu vizuri.

Kiwango cha Awesu dhidi ya Tabora United kama tuzo ya MVP ingekuwa inatolewa kwa mechi moja, Awesu angestahili. Kuna utamaduni mmoja umebadilika kwenye klabu zetu kubwa hapa nchini.

Yanga kiasili ni watu wa mbio nyingi. Mpira wa kasi ambao unategemea zaidi mawinga.

Simba kiasili ni watu wa pasi nyingi fupifupi. Siku za hivi karibuni ni kama Simba wamefuata utamaduni wa Yanga na Yanga wamefuata utamaduni wa Simba.

Wananchi siku hizi wanaupiga mwingi miguuni, Simba wamehamia kwenye mbio. Watu kama Chama na Larry Bwalya ndiyo asili kabisa ya Simba.

Watu kama Pacome Zouzoua ni asili kabisa ya Simba. Mtu kama Luis Miquissone, yule alipaswa kucheza Yanga akiwa kwenye ubora wake.

Siku hizi Yanga ndiyo mafundi wa pira biriani. Msimbazi wamegeuka kuwa watu wa mbio nyingi. Aina ya wachezaji wengi wanaokwenda Simba siku hizi siyo wenye uwezo wa kubeba utamaduni. Nadhani siku hizi kwenye usajili utamaduni wa Simba hauzingatiwi.

Watu kama kina Awesu ni asili kabisa ya utamaduni wa Simba. Bruno Fernandez ni asili kabisa ya Unyamani. Namsubiri kwa hamu Jean Charles Ahoua.

Huyu ni fundi kweli kweli wa boli. Nadhani bado anapambana kuzoea mazingira siku akikaa sawa tutaanza kutafutana. Hapa kuna kila kitu.

Mabao yapo. Mbio zipo na ufundi upo. Amekamilika kwenye kila kitu. Tatizo la mpira wetu ni moja tu. Hatuna uvumilivu. Tunaweza kumkubali mchezaji haraka na kumkataa vivyo hivyo.

Siyo kila mchezaji anaweza kuanza maisha mapya kama Awesu Awesu. Subira wakati mwingine ni muhimu sana kwenye michezo wa soka.

Simba bado haijatulia ukilinganisha na washindani wao wa karibu kwenye ubingwa, Yanga na Azam FC, lakini wanaonekana wana kitu. Simba inaonekana kufanya usajili mzuri wa wachezaji. Baada ya mechi tano za kwanza za ligi, tunaweza kuona mwanga.

Tunaweza kuiona Simba iliyoimarika sawasawa. Kocha wa Simba, Fadlu Davis bado anajaribu kusaka kikosi cha kwanza wakati akipata pia matokeo. Changamoto ya timu kubwa ni kutengeneza timu wakati pia unatakiwa kushinda mechi zako.

Hakuna wa kukuvumilia kama hupati matokeo mazuri. Kitendo cha Simba kwenda misimu minne bila kushinda taji lolote kubwa ni kidonda kibichi kwa viongozi na mashabiki.

Huu ndiyo mwenendo wa timu kubwa. Watu wanataka kuona mpira mwingi na ushindi. Watu wanataka kuona mataji yanarejea Unyamani. Fadlu ana kazı kubwa ya kufanya.

Debora Fernandez, Jean Charles Ahoua, Joshua Mutale na Baba la Baba, Awesu Awesu wana kazi kubwa ya kurudisha furaha ya mashabiki wa Simba iliyopotea. Ni wakati wa kupambania jezi haswa. Bado nina shauku ya kumuangalia tena Awesu akiwa na jezi ya Msimbazi.

Natamani kuona kama atarudia kiwango alichoonyesha dhidi ya Tabora United. Kwa ubora ule akionyesha msimu mzima unaona kabisa kwenye kinyang’anyiro cha MVP, jina la Awesu litaandikwa kwa maandishi makubwa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: