Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amrouche amepanda mtumbwi wa vibwengo?

AmroucheeesAAjl5w.jpeg Kocha Adel Amrouche.

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Filamu isiyoeleweka sana ipo hapa San Pedro. mji ulio kilomita 333 kutoka katika mji mkuu wa Ivory Coast Abidjan. Kila kitu kimetokea hapa kuhusu kocha wa Taifa Stars, Adel Amrouche. Hali ya hewa imechafuka.

Ijumaa jioni ilitangazwa kwamba kocha Amrouche amefungiwa kusimamia mechi nane za Taifa Stars. Kisa? Aliongea ovyo kuhusu taifa la Morocco kuelekea pambano letu dhidi yao Jumatano jioni. Alisema kwamba Morocco wameikamata CAF na wanafanya umafia mbalimbali ikiwamo kujipangia marefa wa kuwapendelea katika mechi zao.

Katika barua hiyo hiyo TFF ikakandamiza kwamba nayo imemsimamisha Amrouche kutokana na kosa hilo hilo. Kuanzia hapo Amrouche akajikuta amepanda mtumbwi wa vibwengo. Kwanini? Kauli yake haikuwa sawa. Ni kweli. Hata kama alikuwa na uhakika na alichoongea, lakini yale yalionekana kama maongezi ya vijiweni.

Kwanza kabisa kabla ya hapo hakupata sapoti kutoka kwa mabosi wake. Rais wa TFF, Wallace Karia alikuwa amemkana hata kabla pambano halijaanza. Lakini chini ya uvungu inaonekana kauli ya Karia ilikuja kutokana na Amrouche kutokuwa na uhusiano mzuri na mabosi wake kwa muda mrefu sasa.

Ilionekana kwamba Amrouche ana dharau kwao. Anaheshimu watu wa juu zaidi hata wale ambao hawapo TFF. Haishangazi kuona Karia alimkana hadharani fasta. Labda alikuwa na kitu moyoni mwake. Ingewezekana kwa TFF kujaribu kurekebisha mambo vizuri zaidi tena chini kwa chini. Ulitegemea CAF wafanye nini baada ya kauli ya Karia?

Lakini ikatajwa kwamba Amrouche hakuwa na uhusiano mzuri na baadhi ya wachezaji. Ikaelezwa kwamba hali ilikuwa mbaya kambini kuelekea michuano hii. Kwamba Amrouche alitaka kuwaondoa baadhi ya mastaa mbalimbali wa Stars kwa sababu zake. Inadaiwa kwamba yupo kambini na wachezaji ambao hata hawaamini na hawataki kwa sababu mbalimbali.

Inasemekana kwamba bila ya mastaa hao kukingiwa vifua na mabosi wa TFF basi nyakati hizi wangeweza kuwa katika kambi za Simba na Yanga popote pale zilipo. Kwa shingo upande alilazimika kuja nao San Pedro kwa ajili ya mapambano haya.

Hata baada ya kumalizika kwa pambano la Stars dhidi ya Morocco wakati waandishi wa habari walipomhoji Mbwana Samatta kama alikuwa haelewani na kocha Amrouche ilitokana na uvumi mwingi uliokuwa umetanda kwa waandishi wa habari waliosafiri Ivory Coast na waliobaki Dar es Salaam kwamba kocha alikuwa haelewani na mastaa wake.

Na sasa imeonekana kama vile Amrouche alikuwa amepanda mtumbwi wa vibwengo baada ya kauli yake kuelekea pambano dhidi ya Morocco. Labda panga lilikuwa linaisubiri shingo yake, huku watazamaji wakiwa na sherehe katika mioyo yao. Labda alikuwa anapigana katika vita ambayo alikuwa peke yake hata kama alikuwa anaamini alikuwa sahihi katika kile alichokisema.

Kwanza bosi wake alimkana, lakini pili bosi wake ni mmoja kati ya watu wenye ushawishi katika viunga vya CAF kwa sasa. Amini usiamini, bosi wake ni mmoja kati ya watu marafiki na wanaoaminika na mabosi wa CAF. Haishangazi kuona Tanzania ni nchi pendwa pale CAF. Michuano ya Super League ilianzia hapa, na pia tumepewa nafasi ya kuandaa michuano ya Afcon mwaka 2027.

Lakini mara baada ya kufungiwa bado TFF ikakandamiza adhabu zaidi kwake. Ni suala tu la kujumlisha moja na moja kisha kujipatia jibu. Karia alikuwa katika nafasi ya kumuokoa, lakini hapo hapo tunaweza kufikiria kwamba alikuwa katika nafasi nzuri ya kukandamiza gongo katika kichwa chake kutokana na kocha mwenyewe kutokuwa na uhusiano mzuri na mabosi wake pamoja na wachezaji mastaa.

Na kuna kitu kingine kimejificha nyuma ya pazia. Nawaza tu. Amrouche alikuwa ametoa kauli kali kwa Morocco huku uhusiano wa taifa lake Algeria na Morocco ukiwa mbovu kuliko wakati mwingine wowote ule. Kumbuka kwamba Morocco ilijitoa katika michuano ya Afcon 2022 kwa sababu za kisiasa.

Michuano hiyo ilifanyika Algeria na Morocco walishindwa kwenda kwa sababu za kiuhasama baina ya mataifa hayo. Ilitafsiriwa kwamba Amrouche alikuwa ametoa kauli hiyo kali dhidi ya Morocco kwa sababu ya utaifa wake. Yeye ni Mualgeria na anahesabika kwamba ana chuki na Morocco.

Wakati Algeria na Morocco wakiwa na uhasama mkubwa hizi ni nyakati ambazo uhusiano wa Tanzania na Morocco umeimarika kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba mataifa haya mawili yamefungua balozi baina yao. Lakini, Morocco wamekuwa wakiisaidia Tanzania katika nyanja mbalimbali.

Katika michezo wamekuwa na uhusiano kiasi kwamba timu za Tanzania zimekuwa zikiweka kambi Morocco. Hapa Amrouche alikuwa ameingia katika mtumbwi mwingine wa vibwengo bila ya kujijua. Kama kulikuwa na uhusiano mwingine mbovu kati yake na watawala au na wachezaji mastaa basi hapa ilipatikana sababu nyingine ya kumuonyesha mlango wa kutokea.

Na sasa ni suala la kusubiri na kuona nini kitaendelea kati ya Amrouche na TFF. Uhusiano wao upo taabani bin hoi, lakini kumbuka TFF haijamfukuza Amrouche. Wakati huo huo kumbuka kwamba mkataba wake na TFF umebakiza mwaka mzima. Anajua kwamba akifukuzwa anapaswa kulipwa pesa nyingi.

Wakati huo huo, TFF inafahamu kwamba Amrouche ana akili za kutosha. Amewahi kushinda kesi mbalimbali za migogoro ya namna hii baada ya kufukuzwa isivyo halali. Mara ya mwisho Wakenya walilazimika kumlipa dola 600,000 baada ya kuwashinda kesi. Walimfukuza kwa njia za panya akawapiga bao CAS ikiamuru alipwe.

Na sasa huu ni mtego kwa TFF na Amrouche mwenyewe. Amrouche ameonyesha nia ya kukata rufaa, lakini unaonyesha vipi nia hiyo wakati unajua wazi kwamba hata askari wako inawezekana hawapo upande wako?  Vyovyote ilivyo, hata kama akishindwa kesi na askari hawapo upande wake sidhani kama atataka mkataba wake uvunjwe.

Akitaka mkataba wake uvunjwe ina maana kwamba hataambulia chochote. Lakini hapo hapo TFF nao sio wajinga. Sidhani kama wanaweza kumfukuza kwa sababu wanajua watakabiliana na majanga ya kumlipa pesa nyingi kocha huyu mjanja. Hata hivyo, wataishi naye kwa muda gani wakiwa katika hali hii?

Kwa wenzetu kuna wakati busara inatumika. Ni makocha wachache wanaopendelea kupokea mshahara bila ya kufanya kazi. Sio utu. Na ni taasisi chache ambazo zinaweza kuwa na furaha kumlipa mshahara mtu asiyefanya kazi. Inapofikia hapo mabosi na kocha hukaa meza moja na kukubali nusu hasara.

Kwa ninachoelewa sidhani kama uhusiano kati ya Amrouche na TFF utarudi kama ulivyokuwa. Kuna yale ambayo TFF inaamini kocha hayupo sawa, ndio maana hawakusimama nyuma yake baada ya kauli yake, na hapo hapo Amrouche anaamini kwamba TFF ilimtosa wakati wa vita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: