Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AFCON 2023 inafikirisha kuliko kawaida

Ivory Coast Yaifurusha Senegal AFCON AFCON 2023 inafikirisha kuliko kawaida

Fri, 2 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mpendwa msomaji ni kawaida ya safu hii kukupitisha katika masuala mbalimbali ya michezo na utamaduni kwa jicho la uchambuzi.

Mara nyingi tumepitia pamoja masuala ya utawala, sheria, masoko, maendeleo na kadhalika. Siyo kawaida safu hii kuongelea matukio ya viwanjani moja kwa moja. Hata hivyo, uwepo wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) yanayoendelea Ivory Coast umeteka macho na masikio ya wapenzi na wasio wapenzi sana wa soka.

Hata hivyo, safu hii imeshindwa kujitenga na msafara wa Ivory Coast, japo si kwa kuangalia matukio moja kwa moja, bali kwa kiasi kikubwa tunaangalia maana ya matukio yanayoendelea Ivory Coast.

Raundi ya timu 16 ya Afcon ilikamilika na tayari timu nane zinapasha misuli moto kuingia katika mchuano wa kupata nne za kucheza nusu fainali ya mashindano hayo makubwa kabisa barani Afrika ambayo mshindi ataingiziwa kwenye akaunti kitita cha takribani Sh18 bilioni.

Kwa mara ya kwanza tangu mashindano yaanze, kama sikosei hakuna timu hata moja ya Afrika Kaskazini iliyoingia robo fainali.

Kwa kifupi ni kwamba timu karibu zote zilizokuwa zikipewa nafasi ya kufika mbali zilianza kuchujwa kuanzia hatua ya makundi na nyingi zaidi ikiwemo mtetezi Senegal, mabingwa mara saba na wana fainali zilizopita Misri, wana nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022, Morocco - wote wameondolewa 16 bora.

Kama nilivyosema awali hii haikuwa kawaida ya mashindano hayo kwani huko nyuma ukifumba macho ulikuwa unaweza kutaja wababe wa Afcon ukianza na mabingwa wa kihistoria Misri ambao msimu huu walifika 16 bora kwa kusuasua. Timu kama Algeria na Tunisia hata ushiriki ni kama haukuonekana kabisa.

Karibu timu zote zilizoingia robo fainali mashindano yaliyopita ya Cameroon 2021 safari hii hazionekani kabisa.

Hakuna aliyetarajia Cape Verde kuwa juu ya Misri, Morocco na Senegal katika hatua hii. Hata wenyeji Ivory Coast wamebaki kwenye michuano kama moja ya miujiza ya ‘tundu la sindano’. Baadhi ya mataifa yaliyoondolewa kama Algeria, Tunisia, Senegal na Morocco yana wachezaji karibu wote wanaochezea klabu za madaraja makubwa huko Ulaya, lakini hawakufua dafu kwa mataifa kama Afrika Kusini yenye wachezaji wawili tu wanaocheza nje ya Afrika.

Kwa kuangalia mchezo wa raundi ya 16 kati ya Morocco na Afrika Kusini ungeweza kusema ni Mamelodi Sundowns inashindana na timu ya dunia. Ilikuwa na kikosi chenye wachezaji wanane kutoka Mamelodi. Ajabu, Morocco hata haikuwategemea wachezaji wanaokipiga kwenye klabu za nyumbani kama Wydad au FAR Rabat. Yote kwa yote Morocco ilikubali kipigo cha mabao 2-0 na pale mwishoni ubao ungeweza kuchafuka zaidi kwa upande wa Morocco.

Wakati upande wa Afrika Kaskazini wakiwa msibani, hali si hivyo Kusini mwa Afrika au Ukanda wa Cosafa. Safari hii Cosafa iliingia na timu nne yaani Afrika Kusini, Angola, Msumbiji na Namibia. Msumbiji ilianza vizuri kwenye kundi kwa kuitangulia Misri 2-1 hadi dakika ya 97 pale VAR iliporuhusu Misri kusawazisha kwa pigo la penalti ya Mo Salah.

Kabla ya mashindano hayo hakuna aliyewapa nafasi Msumbiji.

Msumbiji ilitolewa katika hatua ya makundi, lakini sio kinyonge. Angola imetinga robo fainali kwa kuwaondosha ndugu zao Namibia ambao nao walionyesha kiwango cha hali ya juu. Hakuna asiyejua mipango mizuri ya Cosafa hasa mashindano ya vijana yanayokuwa yakitumika kuibua vipaji vya vijana wa kiume na kike.

Mwaka 2017 nilikuwa mmoja wa makamishna wa CAF katika mashindano ya Afcon ya vijana chini ya miaka 17 yaliyofanyika Gabon. Katika mashindano hayo ambayo timu zilikuwa zinafuzu kwa kujipambania tofauti na mfumo wa sasa wa kuwakilisha kanda, Afrika Kaskazini haikuwakilishwa hata na timu moja.

Sio Misri, Tunisia, Algeria au Morocco zilizokuwa miongoni mwa timu saba ikiwemo Tanzania zilizoungana na wenyeji Gabon.

Hivi sasa ni miaka saba tangu Afcon hiyo ya vijana, jambo hilo linajirudia kwa timu za wakubwa. Bado mtu anaweza kujiuliza kama mpira wa Kaskazini umepiga hatua nyuma au mpira wa Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara umepiga hatua mbele.

Basi tuseme nini? Kwamba mpira wa Afrika kupitia programu mbalimbali hasa zile za maendeleo ya ufundi, vijana na miundombinu zinaanza kuzaa matunda? Kwamba tofauti ya kiuwezo kwa wachezaji wanaocheza nje ya Afrika na wanaocheza nyumbani inazidi kupungua? Kwamba wachezaji wanaocheza Ulaya hawaweki juhudi zote wanapotumikia timu za taifa? Maswali ni mengi, lakini ukweli unabaki kwamba kuna tofauti sana kati ya Afcon ya Ivory Coast na Afcon zilizotangulia. Afcon ya Ivory Coast kwa kiasi kikubwa imekuwa Afcon ya tofauti; Afcon isiyokuwa na mwenyewe.

Wakati wa Kombe la Dunia nchini Qatar 2022, safu hii iliandika kwamba ‘Kombe la Dunia sasa linakuwa Kombe la Dunia’ kwa maana ya kwamba dunia nzima sasa inacheza mpira na tofauti kati ya mataifa na mataifa inaanza kuwa ndogo. Nionavyo na mpira wa Afrika unaelekea huko.

Mpira wa Afrika unaenda kuwa wa Afrika. Kama matokeo ya raundi ya 16 hayatoshi kutuonyesha hilo basi tuangalie mashindano ya vijana na hata mashindano ya klabu ambapo klabu za Kusini mwa Jangwa la Sahara nje ya Afrika Magharibi zinaanza kutunishiana msuli na klabu za Kaskazini. Niko tayari kukosolewa, lakini binafsi sidhani kama mpira wa Morocco, Senegal au Algeria umeanguka ghafla kiasi hicho.

Hii ni Morocco iliyokaribia kucheza fainali ya Kombe la Dunia. Hii ni Algeria yenye wachezaji wa kiwango cha juu kama Riyad Mahrez na wezake wenye kukadiriwa thamani ya pamoja ya zaidi ya Euro 200 milioni, na hii ni Misri yenye Mo Salah na wachezaji wengi wanaowika na klabu ya kihistoria ya Al Ahly.

Hili linakwenda bila kupingwa kwamba mataifa ya Kaskazini kama yalipunguza mwendo katika miradi ya maendeleo ya mpira, basi inapaswa waongeze kasi kwani wapinzani wao wanakimbia wakati wenyewe wanatembea. Sitashangaa na sasa ni dhahiri kwamba timu ambayo haikupewa nafasi kubwa na mashabiki, wachambuzi na wataalamu wa mpira itaweza kuchukua Kombe la mataifa ya Afrika pale kwenye uwanja wa Alassane Ouatara ifikapo Februari 11.

Mwandishi wa makala hii ni mbobevu katika miradi ya maendeleo, utawala na biashara ya michezo na nyanja nyingine. Ametumikia nyadhifa mbalimbali katika asasi za kiraia, kampuni, klabu za mpira, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), CAF na FIFA. Unaweza kumtumia maoni yako kupitia simu yake hapo juu.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: