Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfahamu mzee mwenye wake 22 na watoto 110, hajui idadi ya mabinti zake

E17dafcb 4ddb 4e66 B1cc 28f7f0bbb5dd Mfahamu mzee mwenye wake 22 na watoto 110, hajui idadi ya mabinti zake

Tue, 23 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Inafikirisha namna baadhi ya wanawake wanavyopata wivu pindi waume zao wanapotaka kuongeza mke, lakini si kwa Luhanga Dalushi (72), mfugaji wa mkoani Katavi aliyeoa wake 22.

Mzee Dalushi, anayeishi katika Kitongoji cha Seso wilayani Mpanda, kwa sasa anaishi na wake zake 18 baada ya wanne kuondoka kwa kushindwa kuhimili wivu waliokuwa nao.

Kutoka kwa wanawake hao 18 aliobaki nao, anasema ana watoto 110 na lengo lake ni kuongeza wengine wanne ili kurudi kwenye idadi ileile ya wake 22 aliyokuwa nayo awali, kwani wanakula na kuvaa vizuri bila tatizo lolote.

“Hao wanne waliondoka kwa sababu ya kuwapenda sana. Niliwabana kila sehemu wanakoenda nilitaka kufahamu wanakwenda kufanya nini, niliwaonea wivu. Kutokana na kuwabana kila wanapokwenda waliona kuolewa ni utumwa, wakaachika,” anasema mzee huyo.

Dalushi ni mfugaji anayemiliki ng’ombe 1,800 na tayari wake 18 wameridhia aongeze wengine wanne ili kusaidia kulima na kuilinda mifugo.

Anavyomudu shughuli

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, mzee huyo anasema ili kumudu vyema majukumu yake kama mume na baba ambaye ni kichwa cha familia, amepanga zamu za kulala kwa kila mke.

“Kuna zamu, nalala siku mbili kwa kila mke. Wake zangu waliopo hapa ni sita na hawagombani. Wengine wapo Mtakuja, Sikonge na Mpimbwe,” anasema mzee Dalushi.

“Wake zangu wote wanapendana sana, hakuna baraza tulilokaa kusutana au kuwataka wasigombane. Mke akifika akaona mwenendo tulionao anajiunga na wengine kitabia. Hatuna kugombanagombana kama huko uswahilini,” anasema.

Shughuli kubwa anayofanya mzee huyu pamoja na familia yake ni kilimo na kufuga.

“Makadirio watoto wangu wa kike wanaweza kufika 30 na wengi wameolewa. Watoto wa kiume ni wengi sana, wapo hapa wengine wana familia zao,” anasema.

Kwa nini wake wengi

Akizungumza nyumbani kwake, Dalushi alisema alioa wanawake hao ili kumsaidia kutunza ng’ombe 100 aliowarithi kutoka kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa na watoto 12, yeye akizaliwa wa 11.

Akiwa na miaka 24 tu, mwaka 1974, Mzee Dalushi anasema alioa mke wake wa kwanza na ameendelea kuongeza idadi hiyo mpaka wakafika 22. “Nimezaliwa katika familia yenye watoto 12. Sikubahatika kupata elimu, kwa hiyo sikusoma na sababu ni kukulia katika malezi ya kifugaji, muda mwingi unakuwa maporini ambako hakuna shule,” anasema.

Alipoozeshwa na wazazi wake mwaka 1974, alihama mwaka huohuo kutoka Ushetu mkoani Shinyanga kwenda Mbede Mpimbwe katika Mkoa wa Katavi anakoishi mpaka leo.

Anasema watoto katika familia ya baba yake kila mmoja alipewa urithi wake na alipopewa ng’ombe 100 ilikuwa idadi kubwa ambayo asingeweza kuihudumia akiwa na mke mmoja, hivyo akaongeza wa pili, safari ikaendelea.

Mzee Dalushi anasema ng’ombe hao waliongezeka kabla hajapata watoto wengi, hivyo akaendelea kuoa wake wengine ili kupata nguvu ya kusaidiana kulima na wengine kuchunga mifugo.

“Ndicho kitu kikubwa kilichosababisha mimi kuoa wanawake wengi. Sikupenda kuoa wake wengi isipokuwa kupata nguvu ya kulinda mifugo. Hadi sasa nina ng’ombe 1,800 ila hapa nilipo wapo 600, wengine niliwahamisha,” anasema.

“Nilifanya hivyo baada ya kubanwa na eneo kuwa finyu kwani nazungukwa na Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania) na TFS (Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania) na wakulima kwa hiyo ng’ombe wengine nimewapeleka Lindi na Kigoma,” anaeleza mzee huyo.

Dalushi anasema hadi sasa wazo lake ni kuendelea kuoa wake wengine wanne ili kuziba pengo la walioachika ili wasaidie kudumisha na kuendeleza mali alizonazo.

Mitizamo ya wake zake

Ng’washi Mashishanga, mke wa kwanza wa Dalush anasema ana watoto 11, kati yao aliyekuwa anasoma huko Mpimbwe ni mmoja lakini aliacha alipofika darasa la tano. Anasema mume wake anawahudumia vizuri. “Tunalima na kulea watoto, hatuoneani wivu. Mimi nataka aoe tu mali na chakula vipo hata sasa hivi ameoa mke mwingine hajamaliza mwaka,” alisema Ng’washi akieleza safari ya maisha yao.

Kwa upande wake, Pili Kabendera (30) aliyeolewa mwezi mmoja uliopita alisema anamruhusu mume wake huyo kuoa kwa sababu yeye amewakuta wengine lazima naye akaribishe wengine. “Bado sijapata mtoto ila akitaka kuoa, aoe tu. Najisikia vizuri na haina shida,” alisema Pili.

Changamoto alizonazo

Akizungumzia changamoto zinazomkabili, Dalushi alisema ni watoto wake kutopata elimu kutokana na umbali mpaka shule ilipo, kwani wanahofia kujeruhiwa na wanyama wakali njiani wakati wakienda na kurudi kwa kuwa anaishi porini.

Mbali na watoto wake kutopata elimu, anasema changamoto nyingine ni ufinyu wa eneo la kulima ikilinganishwa na ukubwa wa familia aliyonayo, kwani ana ekari 15 tu. “Mifugo nilikosa sehemu ya kufugia, ndiyo maana nikaigawanya, kero hiyo inaniathiri. Chakula kikiisha nauza mifugo nanunua mazao,” anasema.

“Changamoto nyingine ni ukosefu wa barabara. Tunapata shida usiku tunapotaka kwenda hospitalini. Nimeiomba Serikali ya kijiji iliangalie hilo,” anaeleza Dalushi.

Familia inapopata matatizo ya kiafya anasema huwa wanaenda kutibiwa katika zahanati ya kijiji kwa kutumia pikipiki yake. “Wakiugua wengi tunakodi bodaboda,” anafafanua.

Anasema hakuna tatizo lolote kati yake na jamii inayomzunguka na anaishi nayo vizuri, wanatembeleana na kushiriki maendeleo na kijamii.

Uelewa wa sensa

Mzee Dalushi anasema analima zaidi mahindi na hapati mavuno ya kutosha kutokana na wanyama waharibifu kuvamia shamba lake mara kwa mara. Hata hivyo, anasema kwa msimu huvuna kati ya magunia 60 mpaka 100 kutokana na tembo kuharibu mazao shambani, lakini isingekuwa hivyo, angepata hadi magunia 160.

Mzee Dalushi anasema kwa kuwa familia yake ni kubwa na ipo maeneo tofauti, ameiandaa kikamilifu kuhesabiwa kuanzia mke wa kwanza hadi wa mwisho.

“Kila mmoja na watoto wake watahesabiwa pasipo tatizo lolote na wanaoishi maeneo mengine nimeshawaelekeza,” anasema mzee huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: