Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya kazi yaanza sensa ya watu na makazi

Sensa Mbeya.jpeg Sensa yaanza Jijini Mbeya

Tue, 23 Aug 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati Sensa ya Watu na Makazi ikianza leo Jumanne Agosti 23, 2022, wananchi mkoani hapa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Juma Homera pamoja na viongozi wengine wa Serikali wamejitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa kazi hiyo ya kitaifa.

Uzinduzi wa sensa ya watu na makazi umefanyika usiku wa kuamkia leo Jumanne katika viwanja vya Kabwe jijini hapa, huku makarani na wasimamizi wa shughuli hiyo wakianza majukumu yao kutembelea nyumba kwa nyumba.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Homera amesema sensa ya watu na makazi ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya Taifa huku akiwapongeza wananchi kujitokeza kwa wingi.

Amesema maendeleo huanzia ngazi ya familia ambapo mzazi au mlezi kabla ya kupanga na kuweka bajeti lazima ajue idadi ya watu alionao kwenye familia, hivyo hivyo kwa Taifa lazima ijue idadi ya watu ili kupanga maendeleo.

"Niwashukuru sana kwa muitikio wenu licha ya kuwa ni usiku lakini hii inaonesha dhamira kwamba tunaunga mkono juhudi za serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, naomba tutoe ushirikiano tutakapofikiwa kuhesabiwa" amesema Homera.

Pia, Homera amewahakikishia wananchi taarifa zozote zitakazochukuliwa itakuwa siri na kwamba kila mmoja awe huru kuelezea hali yake ya maisha ili serikali ijue uhalisia wa kila mtanzania.

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema sensa ya watu na makazi ni muhimu kwa kila Mtanzania kuhakikisha anahesabiwa kwa maendeleo ya Taifa.

"Kazi inaanza sahivi hili ni jukumu la kila mmoja, sensa ina umuhimu wake katika kusaidia serikali kujua watu wake ni wangapi ili kupanga mipango ya Maendeleo, niwaombe tushiriki kikamilifu" amesema Maryprisca.

Mmoja ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi huo, Hamis Nurdin amesema yeye na familia yake wapo tayari kuhesabiwa kwani hata yeye bajeti yake huendana na idadi ya watu alionao kwenye familia.

"Ni kama ninavyofanya mimi niwapo kwangu, siwezi kununua kilo 10 za mchele tukapika siku moja wakati ndani tupo wawili, lazima niweke kiwango kulingana na watu tuliopo, hivyo hata hii sensa inahitaji kujua tuko wangapi watanzania ili zile huduma ziweze kutosheleza" amesema Nurdin.

Chanzo: Mwananchi
Related Articles: