Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mara kuna wagonjwa 34 wa Uviko-19

Corona 4?fit=700%2C467&ssl=1 Mara kuna wagonjwa 34 wa Uviko-19

Tue, 17 Aug 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Watu 34 wamelazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Mara wakiugua ugonjwa wa uviko 19.

Akitoa taarifa ya hali ya afya mkoani Mara kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Dk Dorothy Gwajima, Mganga mkuu wa mkoa wa Mara, Dk Juma Mfanga amesema kuwa idadi hiyo ni ya wagonjwa waliopo katika vituo hivyo hadi leo Jumatatu Agosti 16, 2021.

Amesema kuwa kati ya wagonjwa hao wagonjwa saba wapo kwenye mitungi ya gesi ya oksijeni na kwamba taarifa zinaonyesha kuwa maambukizi ya ugonjwa huo yamepungua mkoani Mara ingawa hakutoa takwimu.

Amesema kuwa tangu kuanza kwa chanjo ya ugonjwa wa Uviko 19 mkoani Mara Agosti 5, jumla ya watu 4,856 wamejitokeza na kupata chanjo hiyo na kwamba mkoa unajitahidi kuhakikisha kuwa kila anayetaka kuchanjwa anapata huduma hiyo kwa ukaribu zaidi ambapo vituo vya kutolea chanjo vimeongezwa kutoka 22 vya awali hadi 34.

"Mwitikio wa chanjo kwa mkoa wa Mara ni mzuri hasa ukizingatia kuwa mkoa wetu ulichelewa kuanza kutoa chanjo lakini hadi sasa ni miongini mwa mikoa mitano inayofanya vizuri nchini," amesema Dk Mfanga.

Amesema kuwa mkoa wa Mara una mitungi ya gesi ya oksijeni 62 huku mkoa ukitarajia kupokea msaada wa mitungi zaidi ya 200 kutoka kwa mdau ambaye hakumtaja jina ili kuimarisha huduma za gesi itakapokuwa inahitajika.

Akizungumzia ugonjwa wa Uviko 19 na chanjo yake, Waziri Gwajima amewataka wataalm kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili watu waweze kujitokeza na kupata chanjo huku akisema kuwa tangu kuzinduliwa kwa chanjo hiyo nchini Julai 28, watu wengi wenye uelewa wamejitokeza na kupata chanjo.

"Hata darasani mwalimu anafundisha wapo watakaopewa hapo hapo lakini wapo ambao itawachukua muda kuelewa na wengine inabidi waende twisheni ili waelewe. Kwa hiyo hakuna haja ya kutumia nguvu tuendelee kutoa elimu na pia niwaombe Watanzania wasiwe wepesi wa kudanganywa waingie kwenye mitandao wa wajifunze faida za chanjo," amesema.

Amesema kuwa taarifa zinaonyesha kuwa hivi sasa kuna janga la watu wasiochanjwa ambao ndio wanaongoza kwa kuugua, kulazwa hospitalini na kutumia mitungi ya oksijeni, hivyo Watanzania wapaswa kubadilika na kuachana na taarifa za kupotosha zinazotolewa na watu ambao hawana nia njema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz
Related Articles: