Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madaktari wathibitisha uhakika wa chanjo za COVID-19

Chanjo  Ed Madaktari wathibitisha uhakika wa chanjo za COVID-19

Tue, 10 Aug 2021 Chanzo: Nipashe

*Watoa hofu kuganda damu, wasema haijaripotiwa nchini *Washauri kuacha kunywa siku kadhaa kabla na unapochanja WAKATI Watanzania wakiendelea kupata chanjo ya UVIKO-19 katika vituo maalumu nchini kote, wataalamu na mabingwa wa afya , wanawahimiza wananchi kuchanja na kupuuza sintofahamu kwenye jamii, ambayo inaweza kuwa chanzo cha hofu kwa baadhi ya watu.

Tanzania imepokea msaada wa chanjo aina ya Johnson & Johnson Jensen kutoka Marekani mwezi uliopita iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuchanjwa na kuongoza viongozi wa serikali na wa dini kuchanja.

Licha ya kuanza kutolewa kwa chanjo hiyo, imezuka sintofahamu kutoka kwa wananchi ambayo inaweza kutia hofu, kwa baadhi ya watu kutokuchanja.

Katika kuelimisha jamii, wataalamu wa Wizara ya Afya,, wanakutana na wanahabari mwishoni mwa wiki iliyopita kujibu hoja mbalimbali.

Mkurugenzi wa Kuratibu Utafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini (NIMR), Dk. Paul Kazyoba, anapojibu hoja zinazowatatiza wananchi kama hisia kuwa inaongeza nguvu za kiume, unywaji pombe, muda inapoanza kufanya kazi, akizungumzia pia madhara na faida zake, anaanza na nguvu za kiume.

NGUVU ZA KIUME

Dokta Kazyoba anasema hakuna uhusiano kati ya chanjo na kuongezeka nguvu za kiume huo ni uzushi na kuongeza kuwa hakuna utafiti uliofanywa kuhusu uhusiano wa chanjo ya Johnson & Johnson inayotolewa nchini na kuongeza au kupunguza nguvu za kiume.

“Licha ya kuwa hakuna utafiti kwa sisi wanaume tuliochanja binafsi sikuona mabadiliko yoyote kuhusu nguvu za kiume, kwa maana hiyo naweza kusema chanjo hii haina uhusiano na suala hili,” anasisitiza.

HAMU YA POMBE

Kuhusu unywaji wa pombe, mtaalamu huyo anasema inashauriwa kuwa anayetaka kuchanja asiguse pombe kwa siku tatu kabla na baada ya kuchanja.

“Ni ngumu kumdhibiti mtu mmoja mmoja asinywe pombe, lakini ni muhimu wakazingatia hili hasa kwa vile ikizingatiwa kuwa chanjo haifanyi kazi kwenye mwili wa binadamu mara tu baada ya kuchanja,” anasema Dk. Kazyoba.

Anafafanua kuwa kwa mgonjwa anayekiuka masharti na kunywa pombe kabla na baada ya kuchomwa chanjo, yupo katika hatari ya kupata madhara kwenye ini.

Anasema kwa sababu ini lina kazi ya kuchuja sumu katika mwili wa binadamu hulazimika kuanza kupambana na sumu ya pombe wakati huo huo kupokea chanjo inayoingia mwilini.

ELIMU KUHAMASISHA INAHITAJIKA

Aidha, mbobezi wa Magonjwa ya Ndani na Bingwa wa Figo, Jonathan Mngumi, anasema idadi ya wagonjwa nchini meongezeka hospitalini hivyo ni muhimu wananchi wakaendelea kupata chanjo na waondoe hofu.

Watanzania wanapaswa kuendelea kuelimishwa kuhusu umuhimu wa chanjo, ili waendelee kupata huduma hiyo na kuipunguzia serikali mzigo mkubwa wa matibabu.

Anasema wataalamu wanaendelea kutoa elimu kwa jamii, kujibu maswali ya wananchi, ili wanaopata chanjo wawe na ufahamu wa kutosha na ikitokea amepata shida yoyote aweze kutoa maelezo.

Anasema elimu ikiendelea kuenea maeneo mbalimbali kwa wananchi ni wazi kuwa idadi ya watakaokuwa wanaendelea kuchanja itaongezeka.

“Ndiyo maana leo tumekutana nanyi hapa leo kusaidia kuielimisha jamii, licha ya kuwa jukumu letu ni kutibu, pia ni kuhakikisha tunawakinga watu wasipate magonjwa,” anasema Dk. Mngumi.

HOFU YA KUGANDA DAMU

Akizungumzia suala hilo, Dk. Mngumi anaeleza kuwa athari za kuganda kwa damu kwa watu wanaochoma chanjo hiyo inaweza kutokea kwa asilimia 0.0003 na ambao walionekana awali utafiti uilionyesha walikuwa na shida nyingine zilizosababisha shida hiyo na kuongeza kuwa kama ikitokea aliyechoma chanjo akapata tatizo hilo, japo hapa Tanzania hali hiyo haijaripotiwa, inatibika.

Anasema kila chanjo ina aina yake ya madhara na kwamba wataalamu wanaona kuwa athari zake ni kidogo ikilinganishwa na faida zinazopatikana.

Dokta Mngumi, anazitaja baadhi ya athari za chanjo anazoeleza kuwa ni ndogo ndogo mfano maumivu kwenye eneo alilochomwa, kuchoka kidogo na homa na kuongeza Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) inafuatilia kwa ukaribu taarifa za waliochanjwa na kuwataka wananchi waendelee kujilinda na ugonjwa huo kwa kuzingatia ushauri wa Wizara ya Afya.

“Pia wagonjwa wenye magonjwa sugu ya figo wanashauriwa wapate chanjo hii, ili kuwalinda na UVIKO -19 , chanjo itawalinda hata baada ya kupandikizwa figo,” anashauri.

CHANJO KUANZA KAZI

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mbobezi wa Moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Tatizo Sanga, anasema chanjo huanza kufanya kazi kwenye mwili wa mtu kuanzia siku saba hadi 15.

Anasema baada ya mtu kuchoma chanjo mwili huanza kujipanga kutengeneza utaratibu wa kuipokea jambo linalofanyika ndani ya wiki mbili.

Anasema wakati mtu anapata maudhi madogo madogo yanakuwa ni mashambulizi kati ya kinga za mwili na chanjo inayoingia ndani ya mtu.

“Hiki kinakuwa ni kitu kipya kimeingia kwenye mwili wa binadamu ndiyo maana aliyechoma ataanza kusikia dalili za maudhi fulani fulani kutegemea na mwili wake,” anasema Dk. Sanga.

MAGONJWA SUGU

Kuhusu watu wenye magonjwa sugu kupata chanjo anasema ni muhimu, ili kuwaepusha na mashambulizi ya UVIKO-19 yanayoweza kuwaweka katika hatari tofauti na wasiyo na magonjwa hayo.

“Watu wenye matatizo ya moyo ni muhimu kupata chanjo, ili waepuke changamoto ya upumuaji inayoongeza shambulizi kwenye mwili na kuleta uwezekano wa mgonjwa kupoteza maisha,” anasema Dk. Sanga.

Anafafanua kuwa ni hatari zaidi kwa mtu mwenye magonjwa yasiyoambukiza kama moyo, figo na kisukari wanapopata maambukizi wanakuwa katika hatari ya kupoteza maisha.

“Ndiyo maana tunatoa elimu na kushauri wenye magonjwa sugu kupata chanjo, ili kujikinga na hatari hii,” Anasisitiza.

KUSHAMBULIA MAPAFU

Pauline Chale, Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mbobezi wa Mapafu na Mahututi, anasema virusi vya UVIKO-19 husababisha madhara kwenye mapafu.

Anasema kuna milango ipo kwenye mapafu, moyo, ini na mfumo wa tumbo ambayo ugonjwa huitumia kujishikiza hadi kufika kwenye seli za damu.

Anasema kutokana na muingiliano huo wa kirusi mgonjwa hubanwa mapafu na kushindwa kuvuta hewa na ndiyo sababu ya kumuwekea hewa ya oksijeni ambayo hutumia hadi wiki nne, ili kurejea katika hali ya kawaida.

“Kutokana na kuwa mgonjwa anakaa kwenye oksijeni kwa wiki mbili hadi nne kama hatapoteza maisha, hutumia mitungi mitatu hadi mitano kwa siku. Wakati gharama ya kumlaza mgonjwa mmoja kwa siku ni Sh. 500,000 hivyo utaona gharama zilivyo kubwa kwa mgonjwa anayeugua UVIKO-19,” anasema Dk. Pauline.

Anafafanua zaidi kuwa, mitungi ya gesi inaadimika kwa sababu ya idadi ya aina ya wagonjwa wa mahututi kuongezeka. Anawataka wananchi kuendelea kujikinga na kupata chanjo kwa manufaa yao binafsi na vizazi vyao.

WAJAWAZITO, WANAONYONYESHA

Bingwa wa Mapafu, Grace Shayo, anahimiza wanawake wanaonyonyesha na wajawazito kuendelea kupata chanjo hiyo, kwa sababu haina madhara kwa mtoto anayenyonya au aliyetumboni.

Anasema Shirika la Afya Duniani (WHO), limethibitisha hakuna madhara, hivyo ni muhimu makundi hayo ya wanawake kujitokeza kupata kinga, kwa ajili ya usalama wao na watoto wao.

Anahimiza wanawake wanaonyonyesha kuendelea kutoa huduma ya kunyonyesha watoto wao mara baada ya kuchanja.

“Hata kama wana maambukizi ni vyema wakaendelea kunyonyesha hamna madhara yoyote kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” anasema Dk. Grace.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwisho iliyotolewa na Wizara ya Afya, hadi sasa Tanzania ina wagonjwa 858 wa UVIKO -19, huku vifo vikiwa ni 29.

Chanzo: Nipashe
Related Articles: