Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shahidi: Simu za Mbowe nilizokagua hazikumtaja Sabaya

Mbowefrff Shahidi: Simu za Mbowe nilizokagua hazikumtaja Sabaya

Thu, 20 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa kumi katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu amesema hakuna mahali katika mawasiliano simu zote nne alizopelekewa ofi sini kwake ambapo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya ametajwa.

Aidha katika mahojiano hakuweka wazi iwapo katika uchunguzi wa mawasiliano ya simu alioufanya kuna ujumbe wenye viashiria vya moja kwa moja vya mpango wa kutekeleza makosa ya ugaidi.

Shahidi huyo, Inspekta wa Polisi Innocent Ndowo, alitoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Akijibu maswali ya Dodoso kutoka kwa Wakili wa utetezi Peter Kibatala, shahidi huyo alidai kuwa alichokitoa kwenye ripoti yake ndicho alichokikuta kwenye mawasiliano hayo.

Alipoulizwa kama kuna mahali mawasiliano hayo yalimtaja Sabaya au kupanga kufanya ugaidi Ndowo alidai kuwa barua aliyopokea haikumwelekeza kutafuta taarifa hizo lakini baadaye Kibatala alipotaka kujua iwapo angekaa kimya kama angekuta taarifa za aina hiyo alisema asingeweza kukaa kimya na angeandika kwenye ripoti yake.

Shahidi huyo pia alikaa kimya pale alipoulizwa kama katika mawasiliano hayo kuna mahali alikuta watu wakipanga kulipua madaraja.

Alipoulizwa uwepo wa mawasiliano yoyote yanayozungumzia bunduki aina ya A5340 Luger, Ndowo alimwambia Jaji kuwa Kibatala alikuwa akimuuliza mambo ambayo hakuyafanyia kazi lakini pia alikiri kuwa hakuna mahali miamala ya fedha aliyoiona katika mawasiliano hayo imeeleza kuwa ni kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya ugaidi.

Pia shahidi huyo alishindwa kuekeza ni kwa namna gani aliruhusu vielelezo kuchukuliwa na mtu ambaye siye aliyevipeleka pamoja na kwamba aliileza mahakama kuwa mtu anayepeleka vielelezo ndiye anayepaswa kuvichukua tena kwa kuweka saini katika kitabu maalumu.

Kwa mujibu wa Ndowo vielelezo hivyo vilipelekwa kwake na afande Goodluck wakati aliyevichukua alikuwa afande Swila.

Aidha Ndowo alikana madai ya kuwepo kwa kikundi ndani ya jeshi la Polisi ambacho kilihusika na kupanga njama za kumpa Freeman Mbowe kesi ya ugaidi kama ambavyo Wakili Kibatala alidai.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Khalfan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya ambao wote kwa pamoja wanakabili na mashtaka sita ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kupokea fedha kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya ugaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: