Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Mbeya imesema inaendelea na uchunguzi kubaini ukweli kwa waliokuwa makarani wa sensa, Mtendaji wa Kata ya Sinde, Hawa Kajula na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Mlimani Baita Sanga kwa tuhuma za kupokea rushwa ya Sh 200,000 kila mmoja kutoka kwa watahiniwa wa usahili wa kazi ya sensa ya watu na makazi.
Akizungumza leo Jumatatu, Agosti 22, 2022 wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Maghela Ndimbo amesema kwa sasa wawili hao wapo kwenye kuchunguzwa ili itakapobainika kuhusika wapelekwe mahakamani.
Amesema katika uchunguzi wa awali, ilibainika Mtendaji huyo na Mwalimu, walipokea Sh 200,000 kutoka kwa watahiniwa ambapo TAKUKURU kwa kushirikiana na waajiri walichukua hatua za haraka kwa kuwaondoa pamoja na watahiniwa waliotoa hongo.
"Kwa maana hiyo kwa sasa tunachunguza kwa undani kubaini ukweli ili kuwafikisha mahakamani, niwaombe wote wanaohusika na kazi hii ya sensa kuwa makini kwa kufanya kazi kwa uweledi vinginevyo watakutana na mkono wa sheria, tuko makini kufuatilia kila hatua" amesema Ndimbo.
Mkuu huyo ameongeza kwa kipindi cha siku 90, TAKUKURU mkoani humo ilifanya ufuatiliaji wa miradi ya Maendeleo 11 yenye thamani ya zaidi ya Sh 10 Bilioni ambapo walibaini mapungufu kadhaa katika baadhi yake ikiwamo wakandarasi kuchelewa kuanza kazi katika barabara ya Mbalizi - Mlima reli.
"Kwa kipindi hicho pia tumeendelea na jukumu la kutoa elimu kwa umma kwa makundi yote kuhusu madhara ya rushwa na kupambana kutokomeza vitendo hivyo, niwaombe wananchi kutoa taarifa pale wanapoona au kuhisi harufu ya rushwa sehemu yoyote" amesema Ndimbo.
Pia ameeleza kuwa jumla ya kesi 71 zimeripotiwa za makosa mbalimbali ikiwamo rushwa 49 na 22 za kawaida na kwamba kati ya kesi 15 zilizofunguliwa mahakamani Serikali ilishinda saba na kushindwa tatu.