Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kesi ya Mbowe yatimiza miezi minne

Mbowe Kesipic Kesi ya Mbowe yatimiza miezi minne

Fri, 21 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imesikiliza ushahidi wa mashahidi wa mashahidi 10 wa Jamuhuri katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA , Freeman Mbowe na wenzake wattau kwa miezi minne.

Mahakama hiyo, mbele ya Jaji Joackim Tiganga, jana ilimaliza kusikiliza ushahidi wa shahidi wa 10, Inspekta Innocent Ndowo, na leo inatarajiwa kuendelea na shahidi wa 11.

Inspekta Ndowo ni miongoni mwa mashahidi 24 wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo na vielelezo 19.

Mahakama ilianza kusikiliza ushahidi wa shahidi wa kwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhan Kingai, Septemba 15, mwaka jana. Hadi leo ni miezi minne tangu kesi hiyo ilipoanza kunguruma.

Katika shauri hilo, kuliibuka kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi mara mbili. Mara ya kwanza, jopo la mawakili wa utetezi linaloongozwa na Peter Kibatala, lilipinga kupokewa kwa maelezo ya onyo la mshtakiwa wa pili, Adamu Kasekwa, maarufu kama Adamoo, mbele ya Jaji Mustapha Siyani.

Siyani alikuwa jaji wa pili kusikiliza kesi hiyo baada ya Jaji Elinaza Luvanda kujitoa kutokana na Mbowe kudai kuwa hana imani naye. Kwa sasa Jaji Tiganga anaendelea kusikiliza kesi hiyo baada ya Siyani kuteuliwa kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakaka Kuu.

Mahakama iiliendesha kesi hiyo ndogo huku upande wa Jamhuri ukiwa na mashahidi watatu na upande wa utetezi mashahidi watatu, hivyo jumla ya mashahidi kwa pande zote walikuwa sita.

Kesi ndogo ya mara ya pili ilisikilizwa mbele ya Jaji Tiganga baada ya utetezi kupinga kupokewa maelezo ya onyo la mshtakiwa wa tatu, Mohammed Ling'wenya, kwa madai aliteswa kabla na wakati akichukuliwa maelezo hayo.

Kesi hiyo ndogo ilisikilizwa, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi wanne na upande wa utetezi wakiwa na mashahidi watatu, hivyo kufanya idadi ya mashahidi kuwa saba.

Mahakama katika uamuzi ilipokea maelezo ya onyo ya washtakiwa wote wawili yaliyokuwa yanapingwa, uamuzi wa kesi ndogi ya kwanza ulitolewa Oktoba 20, mwaka jana na uamuzi wa pili ulitolewa Desemba 14, mwaka huo huo.

Katika miezi minne tangu mahakama hiyo ianze kusikiliza, mashahidi wa Jamhuri wamefikia 23 wakiwako 10 wa kesi ya msingi na 13 waliotoa ushahidi kwenye kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.

Leo mahakama hiyo inatarajia kuanza kusikiliza ushahidi wa shahidi wa 11 baada ya shahidi wa 10 kumaliza kutoa ushahidi jana kwa kuhojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.

Wakili Kidando alidai shahidi waliyemtarajia hakufika kwa madai kuwa anatoka nje ya Dar es Salaam na kwamba walimwita shahidi mwingine ambaye alifika jana na wanafanya maandalizi atoe ushahidi leo.

Inspekta Ndowo alipokuwa akimalizia kutoa ushahidi alidai barua iliyopelekwa ofisi ya Tigo kuomba taarifa za miamala na usajili wa simu za washtakiwa, hakutia saini yeye kwa sababu si ofisa mwenye mamlaka.

Alidai mpelelezi ndiye anaweza kubaini mmoja baada ya mwingine kama wanahusika na tuhuma za ugaidi na kwamba nafasi yake kama mchunguzi ni kumpa mpelelezi yale aliyoyaomba.

Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala ambaye alitaka aeleze kama Inspekta muamala upi aliona watu wanapanga tendo la kihalifu na kujibu kwamba hakuna sehemu yenye jambo hilo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Kasekwa, Ling'wenya na Halfani Bwire ambao wanakabiliwa na mashtaka sita likiwamo la kula njama kufanya vitendo vya kigaidi kati ya Mei Mosi na Agosti, 2020.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: