Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

#KESIYAMBOWE: Shahidi aeleza alivyopekua mawasiliano ya Mbowe

B45688290ebe11b0d462c832ef800bbc.jpeg Shahidi aeleza alivyopekua mawasiliano ya Mbowe

Wed, 19 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Shahidi wa 10 katika kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu ameendelea na ushahidi wake jana baada ya hali ya afya yake kutengemaa.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Khalfan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Ling’wenya ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwemo kufadhili vitendo vya ugaidi na kupokea ufadhili kwa ajili ya kutekeleza vitendo hivyo.

Shahidi huyo, Inspekta wa Polisi Innocent Ndowo ambaye ni Ofisa kutoka Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi akishughulika kuchunguza makosa ya kimtandao aliendelea na ushahidi wake mbele ya Jaji Joachim Tiganga kwa kueleza namna alivyofanya uchunguzi wa vifaa ambavyo alivipokea ofisini kwake kutoka katika Jeshi la Polisi.

Ndowo alivitaja vifaa alivyopokea kuwa ni simu nne, mbili zikiwa ni Itel, moja Tecno na nyingine Bundi ambazo alitakiwa kuchunguza mawasiliano yake. Alidai baada ya kupokea simu hizo aliandika barua kwa watoa huduma kuomba taarifa za usajili na miamala ya laini za simu zilizokuwa katika simu hizo na alipozipata aliendelea na uchunguzi wake.

Aliendelea kudai kuwa katika uchunguzi wake alifanikiwa kupata mawasiliano na taarifa za mitandao ya kijamii zilizo fanywa kupitia simu hizo ikiwemo mawasiliano ya Whatsapp, Facebook, Instagram na telegram.

Katika ushahidi wake huo, Ndowo alidai kuwa uchunguzi wake ulimwezesha kuona ujumbe wa mtandao wa whatsapp ambao yalikuwa ni mawasiliano kati ya Freeman Mbowe na Luten Denis Urio lakini pia kati ya Urio na Adam Kasekwa wakielezana hatua mbalimbali za mpango wao wa kutafuta vijana kwa ajili ya kwenda kufanya kazi ya Mbowe.

Akisoma ujumbe baada ya kuwasilisha vielelezo mahakamani, Ndowo alidai moja kati ya mawasiliano aliyoyakuta ni kati ya Mbowe na Urio akimweleza kuwa tayari alishawapata vijana na alitaka atumiwe nauli ili aweze kukutana nao mkoani Morogoro.

Lakini pia alidai kulikuwa na mawasiliano mengine kati ya Urio na Adam Kasekwa ambapo Urio alikuwa anataka kujua kama Kasekwa alifanikiwa kuwashawishi vijana wenzake kwenda kufanya kazi ya Mbowe.

Aliendelea kudai kuwa kulikuwa pia na mawasiliano kati ya Urio na Mbowe wakielezana kuwa vijana walipatikana na walikuwa safarini kuelekea Dar na walikuwa wakiuliza kuhusu mishahara na mahali pa kulala ambapo Mbowe alimhakikishia kuwa hawatatelekezwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: