Ndugu wa waliopoteza maisha kutokana na kimbunga Freddy wamekusanyika jana Jumatano kuwakumbuka na kuwazika wapendwa wao huku Rais Lazarus Chakwera akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia huku idadi ya vifo ikiongezeka zaidi, shirika la habari la VOA Swahili limeripoti.
Kimbunga hicho kilipiga eneo la kusini mwa Afrika kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja mwishoni mwa juma na bado kilikuwa kikisababisha mvua kubwa na kutatiza juhudi za kutoa misaada.
Chakwera aliwaambia waandishi wa habari katika kitongoji cha Chilobwe cha Naotcha, nje kidogo ya mji wa Blantyre “Mimi binafsi nimehuzunishwa sana, wakati mwingine unapopita nje na kuona majeneza mengi hivi huwezi kujizuia kutoa machozi kwa sababu wapendwa, familia nzima imefutiliwa mbali na wengine wengi ambao wameguswa.”
Idara ya usimamizi wa majanga nchini Malawi imesema katika taarifa yake kwamba idadi ya waliofariki kutokana na kimbunga hicho cha pili imeongezeka hadi 225 kutoka 190 huku watu 707 wakijeruhiwa na wengine 41 hawajulikani waliko.