Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi limeanza hii leo Jumanne Agosti 23, 2022, ambapo utulivu katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaama unaonesha muitikio mzuri wa watu kutulia majumbani kuwasubiri Makarani watakaowapa ushirikiano wa kuhesabiwa.
Karani wa Sensa, Mujibu Khalid ameshuhudiwa akiwa katika utekelezaji wake wa majukumu ambapo ilimlazimu kuwaamsha baadhi ya Abiria waliokuwa wamelala katika kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli, ili kuweza kutekeleza zoezi hilo alilolifanya kwa kutumia njia rafiki.
“Samahanani kwa kukusumbua, mimi ni Karani wa Sensa ninaomba unipe ushirikiano kidogo tufanye mahojiano kwa ajili ya sensa ya watu na makazi hasa kwa ninyi ambao mmelala hapa kituoni maana kwa kesho hamtawakuta majumbani kwenu kwa kuwa mnasafiri,” alisema Karani Khalid.
Kama ilivyo katika kazi yeyote, changamoto ni lazima na hapa pia zoezi hili linakumbana na kadhia ambazo hazina ulazima, kijana anayeamshwa na kuhesabiwa anadai yeye atahesabiwa siku zinazofuata na kwamba wamuache aendelee kulala.
“Mimi nipo sisafiri nitahesabiwa asubuhi, naomba tu mniache nipo nitahesabiwa tu,” alisema Mwananchi huyo huku msafiri mwingine Mipao Pilipili akisema hakuna haja ya kukwepa kuhesabiwa na kwamba binafsi alitoa ushirikiano kwa maswali kadhaa aliyoulizwa na Karani na walifanikisha mpango huo.
Kwa upande wa Meneja wa Kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli, akihojiwa na Dar24 amesema zoezi hilo kwa wasafiri waliolala kituoni hapo limeenda vizuri na kwamba hali ya utulivu imetawala na hakuna matatizo yoyote yaliyojitokeza.