Kikosi cha Yanga jana kilizuiwa kufanya mazoezi katika Dimba la Liti mjini Singida ikiwa ni maandalizi yao kuelekea mchezo wa kesho dhidi ya Singida Big Stars.
Hayo yamesemwa na kocha msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze wakati akizungumza na wanahabari mjini Singida kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Tunajua wapo nyumbani kwao, Singida ni timu ambayo imejiimarisha ipo nafasi nzuri kwenye ligi, ina wachezaji wazuri, walimu wazuri, sisi kama Yanga tunahitaji matokeo ili kujihakikishia ubingwa, tumejiandaa kutafuita alama tatu ili kutusogeza kwenye malengo ya klabu msimu huu.
“Mchezo utakuwa mgumu kwenye uwanja mgumu lakini tumejipanga kutafuta alama tatu kesho.
“Ni rahisi kucheza mchezo ukiwa umefuzu kuliko ukiwa umetolewa, hii inakuwa nzuri kwa wazechazaji, morali ya juu, lakini tunapaswa kubadili mtazamo wetu kuondoa mawazo kwenye mechi ya CAF iliyopita na kurejesha akili na nguvu yetu kwenye mechi ya ligi kesho.
“Walituzuia kufanya mazoezi jana kwenye uwanja utakaochezewa mechi tukasema sawa labda na wao wana jambo wamedhamiria, sisi tumejiandaa kucheza na timu yotote ili kupata matokeo,” amesema Kaze.
Hata hivyo, Yanga wamefanya mazoezi yao ya mwisho leo katika uwanja huo tayari kwa kuwavaa walima arizeti wa Singida.