Tulivyocheza dhidi yan DR Congo tulipigwa mabao mawili na mshambuliaji anayeitwa Meshack Elia anayecheza Young Boys ya Uswisi. Zilitosha kutufanya tuondoke vichwa chini kama taifa. Wakongo waliondoka wakicheza zao ndombolo ya solo.
Mwisho wa mechi tulikubaliana kama taifa kwamba Wakongo walikuwa wametuzidi. Wametuzidi wapi? Ukweli ni kwamba walikuwa na wachezaji wanaojua wanachokifanya uwanjani. Walikuwa na wachezaji wenye uzoefu.
Wengi wa wachezaji wale walikuwa wanacheza nje ya taifa lao. Hata waliokuwa katika benchi kama mshambuliaji hatari Fiston Mayele naye anacheza nje ya taifa lake. Msimu uliopita alikuwa mmoja kati ya wafungaji bora katika Ligi Kuu ya Misri.
Beki wao mmoja wa kati, Enock Inonga huwa tumemzoea kiasi kwamba tunamuona kama Mtanzania. Hapana. Sio Mtanzania. Anacheza Ligi Kuu ya Morocco kwa sasa. Kwa hiyo na yeye hachezi DR Congo. Anacheza nje ya taifa lake.
Kuna wakati timu yetu ya taifa inacheza kwa morali nzuri. Haishangazi kuona kwamba katika miaka ya karibuni tumefanikiwa kutinga fainali za Afcon mara mbili. Ilikuwa ni baada ya miaka mingi kupita tangu 1980. Lakini sasa tunajitutumua na kwenda kushiriki.
Hata hivyo, zinakuja nyakati ambazo huwa tunakumbushwa kwamba bado kuna pengo kubwa kati yetu na wenzetu ambao wana wachezaji wengi wanaocheza katika nchi zilizoendelea kisoka nje ya mipaka yao. Ni kama Wakongo walivyokuja kutukumbusha.
Kuna wakati morali inagoma. Kuna wakati mambo ya waheshimiwa kununua tiketi na kuingiza mashabiki wengi uwanjani kushangilia timu huwa yanagoma. Kuna wakati unahitajika ufundi na uzoefu. Bahati mbaya sioni kama tunaweza kufanya zaidi ya tunachofanya kwa sasa.
Sio tukisogea zaidi ya hapa. Mbele kuna giza. Inaanzia kwa wachezaji wenyewe. Wangapi walikuwa na hamu ya kumfuata Mbwana Samatta? Sidhani kama kuna dhamira ya dhati. Matokeo yake Samatta amekuwa mkubwa zaidi kuliko wenzake. Peke yake hawezi kufanya chochote cha maana uwanjani.
Inanikumbusha wakati ule wa George Opong Weah pale Liberia. Wakati mwingine alikuwa analazimika kucheza kama mlinzi wa kati ili aiokoe timu kwa sababu yeye alikuwa mkubwa, lakini wenzake walikuwa wadogo.
Ndoto kubwa kwa vijana wetu ni kucheza Simba na Yanga. Basi. Wachezaji ambao hawatakiwi na Simba na Yanga au na Azam basi ndio walau wanaweza kwenda kucheza nje. Vijana wengi wameua ndoto zao za kucheza nje kwa sababu ya kutakiwa na Simba na Yanga.
Na hapa ndipo pana ugumu. Kama mchezaji akitakiwa na Simba na Yanga na akafanya vizuri katika klabu hizo, basi fahamu kwamba hatauzwa au hataruhusiwa kwenda nje kwa urahisi. Samatta ndiye mzawa aliyepata ngekewa ya kuuzwa kwenda nje kwa sababu Moise Katumbi aliweka mezani kiasi cha pesa ambacho kisingepingika. Lakini leo pia klabu zetu zimejiona zipo katika ushindani mkubwa na klabu nyingine kubwa za Afrika. Kuna mkwamo kwa Clement Mzize kwenda nje kwa sababu Yanga inajiona ipo katika mbio sawa na Waydad Casablanca katika kuwania ubingwa wa Afrika.
Ukiambiwa pesa ambazo Azam wanazihitaji kwa ajili ya kumruhusu Fei Toto kwenda Mamelodi Sundowns unabakia mdomo wazi. Ni kwa sababu Azam inajiona inamhitaji Fei katika mafanikio yake kama ambavyo Mamelodi pia wanamhitaji. Inashangaza kuona sio tu hatuna wachezaji wanaocheza Ulaya, lakini pia hata katika klabu kubwa za Bara la Afrika. Linapokuja pambano la Taifa Stars na DR Congo ndipo tunapokumbuka jambo hili. Pambano likipita tunarudi katika ubishani wetu wa Simba na Yanga.
Klabu hazina sera za kuuza, wachezaji hawana mioyo ya kupambana, lakini pia mameneja wetu wapo tu kwa ajili ya kusubiri kamisheni ya wakati wa usajili hapahapa nchini. Ni meneja gani ana ‘connections’ nzuri za kupeleka wachezaji wake nje? Hapana. Wote wanasubiri Simba na Yanga zipige hodi kwa mchezaji wake.
Baada ya siku za Samatta kuelekea ukingoni huku Simon Msuva naye akipambania dakika zake za mwisho Irak, taifa halina warithi wao. Hayo yanafanyika huku Mayele akiwa anakaa benchi katika kikosi cha DR Congo. Hauwezi kushindana na taifa kama hilo.
Kikubwa utakachosikia ni Pascal Msindo kuongeza mkataba Azam, Mzize kuongeza mkataba Yanga, Edwin Balua kuongeza mkataba mpya Simba. Wenzetu wana wachezaji wanaocheza nje mpaka ndoo yao imejaa. Hauwezi kushindana na watu wa namna hii.
Wakati Misri wakitawala mpira wa ndani wa Afrika walikuwa na ligi ya maana na walikuwa na wachezaji wa maana haswa ambao walikuwa wamefikia viwango vya kucheza Ulaya, lakini wakaamua kubaki nyumbani kwa sababu malipo yalikuwa mazuri. Sisi tuna wachezaji wazuri wa ndani, lakini hawajafikia viwango vya kina Mohamed Aboutrika. Wanahitaji kuendelezwa zaidi.
Hata sasa hivi wachezaji wetu wanaburuzwa zaidi na wachezaji wa kigeni katika timu zao. Hii inaashiria kwamba hatuwezi kuwa kama Misri ile. Hatuwezi kujidanganya. Kama Mzize anaanza katika kikosi cha Taifa Stars halafu Mayele anakaa benchi DR Congo, basi ujue kuna mahala tumekwama kama nchi.
Linganisha tu viwango vya Mzize na Mayele kama wote wangekuwa katika timu moja mpaka sasa. Wakati ule wakiwa pamoja kulikuwa hakuna uwezekano wa Mzize kuanza mbele ya Mayele. Lakini katika timu zao za utaifa unaona wazi kwamba mmoja anakutana na kisiki kikubwa kutokana na nafasi yake kuwa na wachezaji wanaotamba Ulaya. Huyu mwingine hana kisiki kikubwa kwa sababu hakuna wachezaji wa maana katika nafasi yake.