Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yanga yazitaka 3 za Bamako, 3 za Monastir

Wachezaji Yanga 1 1140x640 Yanga yazitaka 3 za Bamako, 3 za Monastir

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kuvuna pointi moja ugenini dhidi ya Real Bamako ya Mali, Yanga imesema kazi kubwa iliyopo mbele yao kwa sasa ni kuvuna alama sita nyumbani katika michezo miwili ijayo.

Yanga juzi iliambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Bamako ugenini, hivyo kufikisha jumla ya pointi nne katika Kundi lake la D la Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa nafasi ya pili nyuma ya US Monastir yenye pointi saba.

Akizungumzia mchezo huo na ijayo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedric Kaze, aliliambia Nipashe kuwa wachezaji walipambana katika mchezo dhidi ya Real Bamako na sasa wanajipanga kwa ajili ya mechi mbili za nyumbani.

Kaze alisema mchezo ulikuwa mgumu na jinsi walivyopambana walikuwa na dhamira ya dhati kuondoka na pointi zote tatu, lakini haikuwa bahati yao baada ya wapinzani kusawazisha dakika za mwisho.

Alisema Real Bamako walicheza vizuri na wachezaji walionekana kucheza kiufundi zaidi na kufanikiwa kutumia upungufu wao kusawazisha.

“Mechi ilikuwa ya ushindani mkubwa, wachezaji walipambana kutafuta pointi tatu ila haikuwa bahati, sasa tumebakiza mechi tatu, mbili za nyumbani tunahitaji kushinda hizo ili kupata nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali.

"Ninaimani na wachezaji wangu tunaweza kufanya vizuri na kufikia malengo ya kucheza robo fainali endapo tukipambana na kupata matokeo mazuri ya ushindi mechi za nyumbani,” alisema Kaze.

Aidha, aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi katika michezo hiyo ya nyumbani ili kutumia vizuri nafasi zao kama mchezaji wa 12 na kwamba benchi la ufundi kazi yake kwa sasa ni kwenda kufanyia kazi kikosi chao kuimarisha zaidi kila idara kuwa fiti.

Mchezo ujao wa Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga itaikaribisha Real Bamako Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumatano ya wiki ijayo kabla ya Machi 19 kushuka tena dimbani hapo kuvaana na wababe wao, US Monastir ya Tunisia.

Yanga itamalizia ugenini mechi zake za hatua ya makundi kwa kucheza na TP Mazembe ambayo mchezo wa awali miamba hiyo ya DR Congo ilikubali kipigo cha mabao 3-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. 

Kikosi cha Yanga kiliondoka jana nchini Mali kuelekea Ethiopia ambapo kitalala hapo kabla ya leo kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: