Benchi la Ufundi la Yanga lililo chini ya Kocha Mkuu Mtunisia, Nasreddine Nabi limepangua mtego waliouweka wapinzani wao Marumo Gallants ya nchini Afrika Kusini ambao hawataamini kitakachowakuta leo.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana katika mchezo wa kwanza ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa leo saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Yanga inahitaji kupata ushindi wa zaidi ya mabao 2-0 ili kupunguza presha watakaporudiana baada ya wiki moja huko ugenini Afrika Kusini.
Mmoja wa mabosi kutoka katika Benchi la Ufundi la Yanga, ameliambia Championi Jumatano kuwa tayari wamepata taarifa za kuwawekea ulinzi wachezaji watatu Fiston Mayele, Stephane Aziz Kii na Bernard Morrison ambaye aliwahi kuichezea Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Bosi huyo alisema kuwa Nabi katika mazoezi yake ya siku tatu Jumamosi, Jumapili na juzi Jumanne alitumia muda mwingi kuwaandaa wachezaji wake wote wanaocheza nafasi ya ushambuliaji, kwani yeyote anaweza kumtumia katika kikosi chake cha kwanza kitakachocheza mchezo huo.