Kuelekea mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Real Bamako, Uongozi wa Yanga umeweka wazi kuwa siku hiyo watakuwa na sapraiz kubwa kwa wanawake wote Tanzania wakiongozwa na Rais Samia Suluhu kwa kuhakikisha wanapata ushindi mkubwa na kutoa zawadi kwa ajili ya siku ya Wanawake Duniani.
Yanga leo Jumatano wanatarajiwa kuwa wenyeji wa Real Bamako katika mchezo wa nne wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga wanarudiana na Bamako baada ya mchezo wa kwanza kuisha kwa sare ya bao 1-1.
Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe alisema: “Baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa kwanza muhimu dhidi ya TP Mazembe katika Uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa, Jumatano tutarejea tena uwanjani kucheza mchezo wetu wa pili nyumbani.
“Mchezo huu kwa bahati ya pekee umeangukia siku ya Wanawake Duniani na kama mnavyojua nchi yetu inaongozwa na mama yetu Rais Samia Suluhu.
“Hivyo kwetu Jumatano tuna sapraiz kubwa kwa Watanzania wote hususani wanawake na tutahakikisha tunaibuka na ushindi wa mabao mengi na kuutoa kama zawadi kwao.”