Licha ya kufanikiwa kufuzu hatua ya Robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya US Monastir, uongozi wa Yanga umechimba mkwara mzito kuwa hawatauchukulia poa mchezo wa mwisho dhidi ya TP Mazembe kwani bado hawajamaliza hesabu zao.
Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga tayari wamekata tiketi ya kucheza robo fainali na wanaongoza msimamo wa Kundi D baada ya kufanikiwa kukusanya pointi 10 wakishuka dimbani mara tano.
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuondoka Tanzania Machi 30, mwaka huu kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa kukamilisha ratiba ya hatua ya makundi watakapovaana na TP Mazembe, Aprili 2, mwaka huu.
Akizungumza nasi, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, alisema: “Sehemu ya kikosi chetu ambacho hakijaitwa kwenye majukumu ya timu za Taifa kinaendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya TP Mazembe utakaopigwa Aprili 2, nchini DR Congo.
“Wengi wanadhani tutauchukulia kwa wepesi mchezo huu kwa kuwa tayari tumeshafuzu hatua ya Robo fainali, lakini niwaweke wazi kuwa bado hatujafunga hesabu zetu, tunataka kuandika rekodi ya kumaliza msimamo tukiwa vinara, hivyo ni lazima tuhakikishe tunashinda mchezo huu.”