Wakati Yanga wakiwa wamebakiza asilimia 50 ya kufanikiwa kutinga katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kuna jambo kubwa kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi pamoja na benchi la ufundi wanalifanya kwa ajili ya msimu ujao wa kimataifa.
Yanga kwa sasa wamebakiza mchezo mmoja wa marudiano dhidi ya Marumo Gallansts huku wakihitaji sare, ushindi au kichapo cha bao 1-0 ili waweze kutinga fainali ya Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.
Katika kuhakikisha kuwa msimu ujao wanaendeleza walipoishia katika michuano ya kimataifa, kocha Nabi ameonekana kuanza safari ya kuanza mapema kusaka majembe mapya kupitia michuano hiyo hiyo ambayo amekuwa akitumia staili ya aina yake.
Imeshuhudiwa kocha Nabi mara kwa mara baada ya michezo kumalizika akifanya mazungumzo na wachezaji ambao wamekuwa wakimvutia akiwa sambamba na meneja wa timu Walter Harryson jambo ambalo ni ishara nzuri kuelekea katika dirisha kubwa la usajili msimu ujao.
Mpaka sasa kwenye michuano ya kimataifa Championi Ijumaa limemnasa kocha Nabi akifanya mazungumzo na wachezaji watatu ambao wote walionekana kuisumbua Yanga na wamefanya vyema katika michuano hiyo kama ifuatavyo.
KATLEGO OTLADISA- MARUMO Mchezaji wa mwisho kwa kocha Nabi kuonekana akizungumza naye ni Katlego Otladisa kutoka Marumo Gallants katika mchezo ambao Yanga walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Katika mchezo huo, Otladisa alikuwa amevaa jezi namba 11, aliwasumbua sana Yanga kutokana na spidi yake na chenga jambo ambalo baada ya mechi kumalizika Nabi alimtuma Meneja Walter Harryson kuzungumza naye na alionekana akimuomba namba yake.
MORRICE CHUKWU – RIVERS UNITED Chukwu ni kiungo mkabaji lakini akiwa anaweza pia kucheza kama kiungo mshambuliaji. Mchezaji huyu baada ya kuonekana kuwavuruga viungo wa Yanga kama kawaida yao Nabi na meneja Walter walizungumza naye kwa dakika mbili jijini Dar.
Hali ambayo ilikuwa sio ya kawaida jambo ambalo liliashiria kuwa walikubali kazi yake huku pia meneja huyo alionekana kuwa na Simu akichukuwa mawasiliano yake.
CHEICKNA DIAKITE – REAL BAMAKO Huyu ni winga wa Real Bamako ambaye katika mchezo ambao Yanga walikuwa ugenini nchini Mali alikiwasha sana kiasi cha Kocha Nabi kuzungumza naye baada ya mpira kumalizika.
Lakini hata baada ya mchezo wa marudiano wakiwa Dar bado kocha Nabi alikwenda tena kuzungumza na mchezaji huyo jambo ambalo lilionyesha kuwa huenda kuna mambo ya usajili yalikuwa yakiendelea kati yao.