Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tanzanite tuko nyuma yenu

0a91d3d5b1efaed82caba9ac0d295a36.jpeg Kikosi cha Timu ya Taifa U20

Sat, 18 Dec 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Leo timu ya soka ya Taifa ya wanawake, Tanzanite ina kazi ngumu dhidi ya wenzao Burundi kwenye mechi ya kuwania kufuzu kombe la dunia kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 20.

Tanzanite itakuwa ugenini, imebakiza hatua chache kufuzu michuano hiyo itakayofanyika Costa Rica mwakani. Ikifuzu itakuwa ni kwa mara ya kwanza kwa Shirikisho la soka Tanzania, TFF kupeleka timu kwenye kombe la dunia. Lakini pia itakuwa ni timu ya pili ndani ya mwaka huu kufuzu kombe la dunia, baada ya timu ya soka ya watu wenye ulemavu, Tembo Warriors kufuzu pia fainali zitakazofanyika Uturuki.

Tanzanite ilishinda mabao 3-2 katika mechi ya kwanza iliyofanyika nyumbani, bado ina kazi ngumu kufuzu, lakini inawezekana wakikazana kama ilivyo kawaida yao. Ili ifuzu Tanzanite inatakiwa kuongeza mabao zaidi lakini ikizuia wenyeji wao wasifunge. Tunafahamu ugumu wa mechi hiyo, tunajua kuwa kutakuwa na figisu za hapa na pale nje na ndani ya uwanja kuwakatisha tamaa wachezaji.

Tunaamini benchi la ufundi na TFF watawajenga kisaikolojia wachezaji hao ili kutambua wanachotakiwa kufanya kuzishinda figisu za wapinzani wao. Tanzanite wajue Watanzania wote tupo nyuma yao, na tunafahamu uwezo wa kushinda mechi hiyo upo kikubwa ni kuwa tayari kukabiliana na mpinzani anayefuata, ambaye hatuna shaka watamshinda na kufuzu. Nafasi hii ni adhimu kwao, tunaimani wanafahamu hilo.

Hivyo ni vema wakatuliza akili zao na kucheza kwa jitihada zote, wakifuzu haitakuwa sifa kwa nchi tu, bali na wao watakuwa wamejisafishia njia ya mafanikio kwani itakuwa mwanzo wa safari ya kuelekea wanakokutaka. Kazi iwe kwenu wachezaji kujituma na kufuatisha yote mliyoelekezwa na benchi lenu la ufundi, mjue nini mnataka na muweke akilini kuwa watanzania wana matarajio makubwa na nyinyi.

Imani kubwa inatokana na ukweli kwamba soka la wanawake halijawahi kutungusha, hivyo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa kufuzu kombe la mataifa Afrika, Afcon, michezo ya All African Games na mingine mingi ambayo timu za wanawake zilifuzu, tunaamini hata kwenye hili la kufuzu kombe la dunia linawezekana.

Hatuna mashaka nao, tunaamini kila jambo linawezekana na bila shaka leo tutapata matokeo ya kufurahisha. Tanzanite nendeni mkarejeshe furaha kwenye sura na mioyo ya watanzania, tuko nyuma yenu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz
Related Articles: