Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameanika mipango yake ya usajili kuelekea msimu ujao kwa kusema amepanga kuongeza wachezaji wachache kwenye kikosi chake ili kufikia malengo.
Tayari kuna taarifa kwamba viongozi wa Yanga wameshamalizana na nyota wawili kuelekea msimu ujao ambao ni winga wa Real Bamako, Cheickna Diakite na nyota kutoka TP Mazembe, Phillippe Kinzumbi.
Akizungumza nasi, Nabi alisema atasajili wachezaji wachache sana ambao watakuja kuongeza nguvu ndani ya Yanga kutokana na kuwa na kikosi kipana ambacho hakihitaji kufumuliwa sana.
“Tutafanya maboresho madogo ya kikosi kwa ajili ya msimu ujao, hakutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwa sababu kikosi kipo vizuri.
“Wachezaji waliokuwepo wana viwango bora, wanaweza kuifikisha timu katika malengo yetu kama tukiongozea baadhi ya wachezaji wachache katika maboresho yangu,” alisema kocha huyo.
Msimu huu, Yanga imefanikiwa kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza, huku ikibakisha hatua chache kutinga fainali ya michuano hiyo.
Mbali na kufanya vizuri kimataifa, katika michuano ya ndani, ipo nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC), huku jana ilitarajiwa kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya pili mfululizo.