Upo uwezekano wa Kocha Mkuu wa Yanga, Mtunisia, Nasreddine Nabi kumuanzisha beki wake Ibrahim Hamad ‘Bacca’ katika kikosi chake cha kwanza kitakachoanza dhidi ya US Monastir ya nchini Tunisia akichukua nafasi ya Bakari Mwamnyeto.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Jumapili hii saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa tano wa hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Beki huyo huenda ukawa mchezo wake wa kwanza kuanza kikosi cha kwanza cha Nabi katika michuano hiyo mikubwa Afrika.
Taarifa ambazo tumezipata, kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la timu hiyo, kocha huyo analazimika kumuanzisha katika mchezo huo baada ya kukosekana Mwamnyeto mwenye majeraha ya goti.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Nabi alianza muda mrefu kumuandaa beki huyo kwa kumchezesha pamoja na Dickson Job tangu katika mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports waliocheza dhidi ya Geita Gold kwa lengo la kutengeneza muunganiko.
Aliongeza kuwa kocha huyo aliendelea kuwaandaa Bacca na Job kucheza pamoja mazoezini huko kambini Kijiji cha Avic Town, Kigamboni Dar ili kuhakikisha wanaelewana.
“US Monastir wanatarajiwa kukutana na sapraizi ya baadhi ya wachezaji kuanza katika kikosi cha kwanza ambao hawajawaona katika mchezo wa awali tuliocheza nyumbani kwao Tunisia.
“Sapraizi ya kwanza watakayokutana nayo ni beki wetu Bacca ambaye huenda akaanza katika kikosi cha kwanza akichukua nafasi ya Mwamnyeto ambaye yeye upo uwezekano mkubwa wa kutokuwepo kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata dhidi ya Real Bamako.
“Hivyo kocha Nabi ameangalia mabeki wake wote na kumchagua Bacca ambaye huenda akaanza kucheza pamoja na Job ambao alianza kuwatumia kucheza pamoja katika mchezo dhidi ya Geita Gold,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo Nabi alisema kuwa: “Nina kikosi kipana cha wachezaji wengi wenye ubora, hivyo kama akikosekana mmoja anakuwepo mwingine mbadala wake mwenye uwezo kama wake.
“Nafurahia kuwa na wachezaji wa aina hiyo katika timu, hiyo ndio sababu ya sisi kupata matokeo mazuri katika michezo yetu.”