Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema kuwa mbinu aliyoitumia kuwakabili Rivers United katika mchezo wao wa marudiano ilikuwa ni kujilinda zaidi kuliko kushambulia.
Nabi amesema hayo mara baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuiondoa Rivers United ya Nigeria.
“Kama nilivyosema awali kabla ya mechi, hawa jamaa hawakuwa na chochote cha kupoteza, hivyo lazima mechi ingekuwa kama ilivyokuwa, ndio maana nilibadilisha kikosi ikabidi nicheze na mabeki wawili wa pembenei ambao watakaba sana kuliko kushambulia.
“Ndio maana Djuma Shaban na Lomalisa nikawaweka nje nikaanza na Kibwana na Dickson Job, pia nikaanza na viungo wenye asili ya kukaba ili watusaidie kukaba na tukipata nafasi ya kupitisha tutafute bao huku tukijilinda. Kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi mbili na kipindi cha pili nafasi tatu lakini zote hatukuzifanyia kazi.
“Tulikuwa tunahitaji kushinda lakini hata kama hatukushinda sio mbaya, ilikuwa mechi nzuri na tumejitahidi kuwazuia wapinzani wetu wasipate bao. Tulitamani kushinda ila ndiyo hivyo hatujapata bao.
“Mechi iliyopita tulipata mabao mawili, leo tulipata nafasi ya kupata mabao matano lakini hatukufanikiwa, hiyo inatokea kwenye mechi. Tungesema tucheze kwa kufunguka kipindi cha kwanza tungewapa mwanya wa kutushambulia na wangetufunga kipindi cha kwanza wangerudi mchezoni, wangetufunga bao la pili na mechi ingekuwa ngumu kwetu.
“Mechi na namna hii unatakiwa kucheza kwa akili na mbinu kubwa mno, ndiyo maana tumetumia muda mwingi kujilinda zaidi ili tuweze kufuzu kwa mtaji wa mabao ya mechi ya kwanza” amesema Nabi.
Yanga itakutana na Marumo Gallants katika hatua ya nusu fainali ambapo mchezo wa kwanza utapigwa katika dimba la Mkapa, Mei 10, 2023 kisha mchezo wa marudiano utapigwa nchini Afrika Kusini Mei 17, mwaka huu.