Kuelekea mchezo mkali wa Kariakoo Dabi ambao unawakutanisha majayanti wa soka la Tanzania, Simba na Yanga utakaopigwa Jumapili hii, uongozi wa Yanga umetamba kuwa walimpa muda mrefu wa kupumzika Bernard Morrison kwa ajili ya kazi maalum atakayoifanya kwenye mchezo huo wa Jumapili.
Simba Jumapili wanatarajiwa kuwakaribisha Yanga katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam ambapo timu zote mbili zinaingia katika mchezo huo zikiwa na kumbukumbu ya matokeo ya sare ya bao 1-1 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Oktoba 23, mwaka jana.
Kuelekea mchezo huo Yanga wanaingia wakiwa na faida kubwa ya kurejea kwa baadhi ya mastaa wao muhimu ambao walikuwa na majeraha miongoni mwao akiwa ni kiungo Mghana, Morrison ambaye katika mchezo wa mwisho dhidi ya Kagera Sugar alifunga bao moja kwenye ushindi wa mabao 5-0 Jumanne wiki hii.
Akizungumza nasi, Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema: “Tunajua utakuwa mchezo mgumu kutokana na ubora wa Simba, lakini tunajivunia ubora wetu kama kikosi, lakini jambo kubwa zaidi kurejea kwa baadhi ya wachezaji wetu muhimu walikuwa mna majeraha.
“Mchezaji kama Morison alikuwa nje kwa muda mrefu na tulimpa muda mwingi wa kupumzika ilia pone kabisa na kuelekea mchezo hu ni miongoni mwa wachezaji ambao wana kazi maalum.”