Kwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitupa nje Rivers United, Yanga imeandika historia ya kibabe katika soka la Tanzania lakini wakati ikifanya hivyo, nyota wake Fiston Mayele naye ameweka rekodi ambayo watani wao Simba hawatopenda kuisikia.
Mayele ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa timu ya Tanzania aliyefunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika mashindano ya klabu Afrika, kuanzia hatua ya makundi na kuendelea.
Nyota huyo kutoka DR Congo, amefikia rekodi ya Mrisho Ngassa ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Yanga katika mashindano ya klabu Afrika na amefikisha idadi ya mabao 12 hivyo kama akipata angalau bao moja katika mechi zilizo mbele yao, ataipiku na kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Yanga katika mashindano ya klabu Afrika.
Mayele alifunga mabao matatu katika hatua ya makundi dhidi ya Real Bamako na Monastir na mabao mawili alipachika dhidi ya Rivers United katika mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali waliyoibuka na usindi wa mabao 2-0 ugenini huku Nigeria.
Mayele amewapiku Clatous Chama na Jean Baleke wa Simba ambao kila mmoja alipachika mabao manne ambayo yalikuwa ni idadi kubwa zaidi kuanzia hatua ya makundi na kuendelea lakini bado ana nafasi ya kuboresha zaidi rekodi yake na kuwapa mlima mrefu wa kuivunja wachezaji wengine, kwa vile Yanga bado imebakia katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga imeweka historia ya kuwa ya kwanza Tanzania kufanikiwa katika miundo mipya ya mashindano ya klabu Afrika iwe katika Ligi ya Mabingwa Afrika au Kombe la Shirikisho Afrika.
Kumbukumbu inaonyesha, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufanya mabadiliko ya muundo wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1997 na kuanza kuitwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na yalianza kuwa na hatua ya makundi, Yanga ndio ilikuwa timu ya kwanza kutinga hatua ya makundi ilipoanza kuwepo rasmi mwaka 1998 huku watani zao, Simba wakifuata nyayo mwaka 2003.
Mwaka 2004, CAF ilifanya marekebisho ya mashindano yake mawili, Kombe la CAF na Kombe la Washindi na iliyaunganisha na kufanya kuwa shindano moja lililoitwa Kombe la Shirikisho Afrika na Yanga ikawa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo, mwaka 2016 na 2018.
Pia Yanga ndiyo timu ya kwanza ya Tanzania kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya klabu Afrika tangu CAF ilipofanya marekebisho ya muundo wa mashindano yake mwaka 2017 na iliongeza hatua ya robo fainali baada ya makundi, kisha kufuatiwa na fainali tofauti na hapo awali na baada ya mechi za hatua ya makundi, hakukuwepo na hatua ya robo fainali.
Akizungumzia mafanikio hayo, Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema kwa sasa akili yao wanaielekeza katika hatua ya nusu fainali ambayo watacheza na Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
"Ni jambo la kufurahisha kuona tumefuzu nusu fainali lakini bado tuna jukumu liko mbele yetu ambalo ni kufanya vizuri kwenye nusu fainali na kwenda fainali. Nawapongeza wachezaji wangu kwa kazi nzuri waliyoifanya na sasa tunajipanga kwa hatua inayofuata," alisema Nabi.