Mshambuliaji kinara wa Yanga, Fiston Mayele amewapa ujumbe watu wanaoibeza klabu hiyo na kusema wamebahatisha kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Mayele amesema hayo jijini Dar mara baada ya kuwasili nchini na kikosi hicho wakitokea Algeria ambako walikuwa wakicheza fainali hiyo ambapo USM Alger waliibuka mabingwa wa michuano hiyo juzi Jumamosi, Juni 3, 2023.
Aidha, Mayele amewapongeza wachezaji wenzake kwa kujituma kwa bidi na kuhakikisha wanafikia malengo waliokuwa wamejiwekea katika msimu huu.
“Kabla ya kusafiri nilisema tunaenda kupamabana na kuhakikisha tunarudi na ushindi, tulitakiwa kushinda bao 2 na tulifanikiwa kupata goli la mapema sana dakika ya 7 na tukaendelea kupambana tena kutafuta bao la pili lakini hatukufanikiwa.
“Kiukweli tulikuta mazingira magumu sana lakini haiwezi kuwa sababu. Muda ambao tulikuwa tukishambulia na wao walikuwa na mipango yao ya kurusha mipira mwili miwili uwanjani, kupiga mafataki, tunasimama tunapoa lazima kutafuta tena namna ya kushambulia.
“Binafsi ninawapongeza sana wachezaji wenzangu kwa sababu tumepambana sana tangu tuanze mashindano haya mpaka leo.
“Watu ambao wanasema Yanga imebahatisha kufika fainali sio jambo zuri kwa sababu ukiangalia namna ambavyo tulianza na timu ilipofikia, utaona watu walivyopambana kwa nguvu zote kufikia hapa.
“Tunamshukuru Mungu kwa kila jambo, tumekosa kombe lakini hatujui mwakani Mungu ametuandalia nini, sababu mimi nina mfano mwaka jana nilikosa kiatu cha Ligi Kuu ya NBC lakini leo nachukua kiatu cha CAF, Mungu ana mipango yake,” amesema Mayele.