Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mayele anataka heshima Simba

Mayele Mweh Mayele

Fri, 14 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kushindwa kuifunga Simba kwenye mechi tatu za ligi, mshambuliaji wa Yanga Mkongomani Fiston Mayele sasa ameapa kuvunja mwiko huo na kuweka rekodi ikiwemo kulipatia chama lake ushindi katika mechi itakayozikutanisha timu hizo mbili, 'Kariakoo Derby' Jumapili ijayo, April 16 mwaka huu uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mayele tangu amejiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu uliopita amekutana na Simba mara sita na kuifunga mabao matatu lakini yote yakiwa katika Ngao ya Jamii na sio ligi.

Nyota huyo anayeongoza kwa mabao hadi sasa kwenye ligi akifunga mara 16, alianza kuifunga Simba bao moja na la ushindi kwa Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii msimu uliopita iliyomalizika kwa matokeo ya 0-1, baada ya hapo zilichezwa mechi mbili za ligi katika msimu huo na zote kumalizika kwa suluhu.

Baada ya hapo timu hizo mbili zilikutana tena Mei 28 mwaka jana katika mechi ya kombe la TFF (ASFC) na Yanga kushinda 1-0 kwa bao la Feisal Salum 'Fei Toto', kisha zikakutana tena Agosti 13 mwaka jana katika Ngao ya Jamii ndipo Mayele akafunga mabao mawili yaliyoipa Yanga ushindi baada ya kutanguliwa kwa bao la Pape Sakho na mechi kumalizika Simba ikipoteza kwa 2-1.

Mechi iliyofuata ilikuwa ya mzunguko wa kwanza wa ligi msimu huu iliyopigwa Oktoba 23 mwaka jana na kumalizika kwa sare ya mabao 1-1 yaliyofungwa na Agustine Okrah (Simba) na Yanga kusawazisha kupitia kwa Stephane Aziz Ki aliyefunga kwa frikiki ya moja kwa moja na mechi ya marudiano ni hiyo ya Jumapili ambayo Mayele amesema anataka kuifunga Simba kwenye ligi na kubakiza Ruvu Shooting na Tanzania Prisons kuwa timu pekee ambazo hajazifunga kwenye ligi tangu atue bongo.

"Dabi mara zote haitabiliki na inakuwa mechi ngumu, kwa upande wetu tunataka kushinda ili kuweka heshima lakini pia kufikia malengo ya kutetea ubingwa msimu huu, binafsi sijawahi kuifunga Simba kwenye ligi licha ya kwamba nimewafunga mabao matatu katika Ngao ya Jamii, nadhani huu ndio wakati wangu kufanya hivyo na namini nikipata nafasi nitafunga na kuweka rekodi vizuri," alisema Mayele.

Aidha Straika huyo alizungumzia bao lake la juzi dhidi ya Geita Gold kumuongezea morali baada ya kutofunga muda mrefu kwenye ligi ikiwa mara ya mwisho alifunga bao moja na la ushindi kwa Yanga kwenye mechi dhidi ya Ihefu iliyopigwa Januari 16, mwaka huu kwa Mkapa na kumalizika kwa matokeo ya 1-0.

"Ni muda kweli nilikuwa sijafunga kwenye ligi lakini nilifunga katika mashindano mengine, lakini pia hata ambavyo nilikuwa sifungi katika ligi, timu ilifanya vizuri na wengine walifunga jambo ambalo linaonyesha ukubwa wa timu yetu nadhani bao hilo litaniongezea hali ya kujiamini na nitaendelea kufunga kila nikipata nafasi," alisema Mayele mwenye ndoto za kuwa mfungaji bora msimu huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: