Mshambuliaji wa Yanga, Fiston Kalala Mayele amesema kuwa kuitwa kwake katika Timu ya Taifa ya Congo DR ni bahati kubwa kwa taifa hilo linawachezaji wengi wazuri hasa katika nafasi anayocheza yeye.
Mayele ambaye ndiye kinara wa mabao katika klabu ya Yanga, amefunguka hayo mara baada ya klabu hiyo kufanikiwa kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Monastir ya Tunisia kwa bao 2-0 katika Dimba la Mkapa, juzi Jumapili, Machi 19, 2023.
“Nina furaha kubwa sana kuitwa Timu ya Taifa ya Congo, nyie mnafahamu wacheaji wa timu ya Taifa, beki au kiungo unaweza kuitwa timu ya Taifa lakini mshambuliaji ni vigumu sana kwa sababu Congo ina washambuliaji wengi wazuri na wanacheza timu kubwa, ligi kubwa na mashindano makubwa.
“Kwa mara ya kwanza naitwa timu ya taifa, ninawashukuru Eng. Hersi (Rais wa Yanga), Said Ghalib (Mwekezaji wa Yanga - GSM) na benchi la ufundi na wachezaji wote kwa sababu wamenisapoti kwa miaka yote miwili tangu nimekuja Yanga, kwakweli nawapenda sana. Mungu akipenda nitatetema,” amesema Mayele.
Mchezaji huyo aambaye ameitwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Congo kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha yake, tayari ameshawasili nchini kwao kwa ajili ya kujiunga na kambi ya timu yake ya taifa kujiandaa na mchezo wa kusaka kufuzu fainali za AFCON 2023 dhidi ya Mauritania, Machi 24, 2023.