Licha ya Yanga Jumamosi wiki hii kukabiliwa na mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka la Azam (ASFC), maarufu Kombe la FA dhidi ya Geita Gold FC, mshambuliaji na kinara wa mabao wa timu hiyo, Fiston Mayele, amesema akili na hesabu zake ni kutetema dhidi ya Simba Aprili 16, mwaka huu.
Mayele ambaye mchezo uliopita wa Ligi Kuu raundi ya kwanza dhidi ya Simba alishindwa kuziona nyavu, hivyo kukosa fursa ya kushangilia kwa staili yake ya kutetema, amesema mchezo wao dhidi ya Simba utakuwa mgumu jambo ambalo linamfanya kuwa na kazi ya ziada ya ili kutimiza azma yake hiyo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi, alisema kwa sasa anauwazia mchezo huo licha ya kwamba mechi iliyopo mbele yao ni dhidi ya Geita Gold kwenye Kombe la FA na kisha Kagera Sugar katika mechi ya Ligi Kuu kabla ya kuivaa Simba.
Baada ya mchezo huo dhidi ya Geita Gold, Yanga itashuka tena Uwanja wa Azam Complex Jumanne ya wiki ijayo kuikaribisha Kagera Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu kabla ya Aprili 16, mwaka huu kuifuata Simba katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika mchezo uliopita wa ligi hiyo, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 shukrani kwa wafungaji Agustine Okrah aliyeitanguliza Simba kabla ya Stephano Aziz Ki kuisawazishia Yanga.
Hivyo, Mayele amesema mikakati yake ni kutetema katika mchezo huo ili atimize malengo yake ya kumaliza msimu huu akiwa ameifunga Simba.
"Mchezo wa Simba na Yanga huwa mgumu, nitahakikisha napambana kuipa ushindi timu yangu kwenye mchezo huo nikishirikiana na wachezaji wenzangu.
"Ninataka nimalize msimu huu nikiwa nimeifunga Simba, naamini hakuna kitakachoshindikana ukiwa na malengo," alisema Mayele.
Alisema anashukuru ushirikiano wanaopewa na mashabiki wao kwenye kila mchezo wanaoucheza ukiwamo ule wa Kombe la Shirikisho Afrika uliomalizika hivi karibuni dhidi ya TP Mazembe, Lubumbashi nchini DR Congo.
Mayele alisema wanaingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Geita Gold, watakaoucheza Jumamosi, ukifuatiwa na wa Ligi Kuu ambao watakutana na Kagera Sugar Aprili 11,kabla ya kukutana na watani wao, Simba.
Yanga itashuka dimbani dhidi ya Geita Gold ikiwa na nia ya kupata ushindi ili kuendelea katika mbio za kutetea taji hilo la FA na endapo itashinda itakutana na Singida Big Stars katika hatua ya nusu fainali.
Kwa upande wa Ligi Kuu Bara, Yanga ambayo ni mabingwa watetezi, wapo kileleni wakiwa na alama 65, nane zaidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili wakati huu timu hizo kila moja ikiwa tayari imeshuka dimbani mara 24.