Tunataka pointi tatu. Kocha msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze amesema hakuna lugha tofauti na hiyo kambini kwao. Yanga itakuwa ugenini dhidi ya Simba leo jioni, kwenye mchezo wa ligi dhidi ya watani zao Jumapili huku wakishuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya sare ya bao 1-1 kwenye mchezo wa kwanza.
Akizungumza nasi alisema wataingia kwa kuwaheshimu wapinzani wao wakiwa tayari wamefanya maandalizi ya kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo huo ambao ameweka wazi kuwa dakika 90 zitaamua ubora kwa timu itakayopata matokeo.
"Wachezaji wameahidi kufanya vizuri kwenye mchezo huo sisi kama benchi la ufundi pia tunaendelea kuwaweka fiti wachezaji wetu ili kuweza kupata matokeo ambayo yatatupa heshimba mbali na taji ambalo tuna asilimia kubwa ya kulitetea;
"Mechi ya Simba na Yanga imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka hii ni kutokana na timu hizo mbili kufanikiwa kukusanya mashabiki wengi na ndio mechi ya heshima hivyo tunataka kupata pointi tatu ambazo zitasindikiza ubingwa msimu huu."
"Simba ina wachezaji wengi wazuri ambao wanaweza kutupa changamoto hilo tumejipanga nalo kwenye kiwanja cha mazoezi kuhakikisha tunawapa wakati mgumu kwa kuwadhibiti ili kujirahisishia njia ya kupata matokeo ya ushindi;
"Tukipata pointi tatu kutoka kwa watani zetu itakuwa ni heshima kubwa kwa benchi la ufundi na ubingwa wetu tutakapofanikiwa kuutetea kwani soka la Tanzania hweshima ni kumfunga mtani mbali na mafanikio ya kutwaa taji." alisema kaze.
Akizungumzia majeruhi kwenye kikosi chao alisema kwa asilimia kubwa wachezaji wao wote wapo kwenye hali nzuri na wameweza kufanya mazoezi. "Hatuna mchezaji ambaye anaweza kukosekana kwenye mchezo wa Jumapili japo siwezi kulithibitisha hili kwakuwa bado tuna siku moja kabla ya mchezo Mungu ndiye anajua kesho ya mtu na sio mwanadamu." alisema Kaze ambaye ni raia wa Burundi.