Kiungo Mkabaji wa Rivers United ya nchini Nigeria, Joseph Onoja, amesema kuwa, kama akifanikiwa kutua Simba, basi yupo tayari kupambania namba mbele ya Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin.
Mnigeria huyo aliingia katika kikosi bora cha mchezo wa tano wa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na wachezaji watatu wa Simba, Jean Baleke, Clatous Chama na Kanoute.
Kiungo huyo ni kati ya nyota wanaotajwa kuwa katika orodha ya wachezaji wanaowaniwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao.
Akizungumza nasi, Onoja alisema anaamini kiwango alichonacho, hivyo kama mipango ya kujiunga na Simba itakamilika, basi hatakubali kukaa benchi na badala yake ataingia katika kikosi cha kwanza.
Onoja alisema anaheshimu ubora na kiwango cha kila mchezaji ndani ya Simba, lakini hiyo haimfanyi aogope kupambania namba na kuingia katika kikosi cha kwanza.
“Mimi nimezaliwa kupambana, kila sehemu nilipokwenda kucheza nimekuwa nikikutana ushindani wa namba ambao unanifanya niongeze bidii ya kupambana ili niingie katika kikosi cha kwanza.
“Simba ninaifahamu na nimekuwa nikiifutilia kwa karibu, nawafahamu wachezaji baadhi katika timu hiyo, ambayo ninaamini nikijiunga nayo basi nitaingia katika kikosi cha kwanza,” alisema Onoja.
Upo uwezekano mkubwa wa Simba kuachana na kiungo wake Ismail Sawadogo aliyejiunga na timu hiyo katika usajili wa dirisha dogo msimu huu baada ya mchezaji huyo kushindwa kuonesha upinzani mbele ya Mzamiru na Kanoute.