Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hawa ndo Kaizer Chief sasa

Kaizer Chiefs Dar Hawa ndo Kaizer Chief sasa

Sat, 22 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Yanga leo Jumamosi inahitimisha Kilele cha Wiki ya Mwananchi, likiwa ni tamasha la tano kwa klabu hiyo tangu ilipoasisi wiki hiyo mwaka 2019.

Katika tamasha hilo ambalo safari hii limepangwa kufanyika Julai 22, tofauti na msimu uliopita lilipofanyika Agosti, litawapa nafasi viongozi, wanachama, mashabiki sambamba na wapenzi wa Yanga kujumuika pamoja ili kupata burudani na kushuhudia utambulisho wa kikosi kipya.

Mbali na burudani tamu ya muziki kutoka kwa wasanii mbalimbali waliopangwa kutumbuiza katika tamasha hilo lililoasisiwa na uongozi wa Dk. Mshindo Msolla na Fredrick Mwakalebela, pia huwa kuna pambano la soka la kirafiki la kimataifa la kuhitimisha kilele hicho.

Safari hii Yanga imeialika Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ili kujipima ubavu juu ya kikosi hicho kama Mwanaspoti linakudadavulia wasifu wa AmaKhosi moja ya klabu kubwa ya Sauzi ikila sahani moja na Orlando Pirates moja ya klabu kongwe nchini humo.

KUASISIWA

Wakati Yanga ikiwa na miaka 88 tangu ilipoanzishwa mwaka 1935, kwa wapinzani wao Kaizer Chiefs ni tofauti kwani klabu hiyo ndio kwanza imetimiza miaka 53 tangu ilipoanzishwa Januari 7, 1970.

Kaizer iliyoko Naturena huko Kusini mwa Johannesburg hufahamika kwa jila la utani la 'AmaKhosi' ambalo limebeba maana ya 'Lords' (bwana), 'Chiefs' lenye maana ya kiongozi au mtawala mkuu wa kizulu.

MMILIKI

Mmiliki wa timu hii ni Kaizer Motaung aliyewahi kuwa mchezaji na kwenye kiongozi wa Chama cha Soka cha Afrika Kusini akiwa ndiye mwanzilishi, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo.

Motaung aliyezaliwa Afrika Kusini Oktoba 16, 1944, amewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo, Orlando Pirates, Atlanta Chiefs na Denver Dynamos huku akifahamika kwa jina la utani la 'Chincha Guluva'.

KOCHA MKUU

Kocha mkuu wa kikosi hichi ni Molefi Ntseki aliyeteuliwa Juni 29, mwaka huu kuchukua nafasi ya Arthur Zwane aliyeshushwa cheo na kupewa cha ukocha msaidizi akishirikiana na Dillon Sheppard.

Ntseki aliyewahi kuifundisha timu ya taifa ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana' kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, kabla ya kupewa kocha mkuu alihudumu kama Mkurugenzi wa Ufundi na maendeleo ya Soka la vijana.

Kabla ya Ntseki kula shavu, mabosi wa klabu hiyo walikuwa wakimnyemelea Nasreddine Nabi aliyeachana na Yanga baada ya kumaliza mkataba, lakini mazungumzo yao yalishindwa kupata muafaka na AmaKhosi kumbeba kocha huyo, huku Nabi akiibukia AS FAR Rabat ya Morocco.

MATAJI 12

Wakati Yanga ikijivunia mataji 29 ya Ligi Kuu Bara nchini, kwa wapinzani wao Kaizer Chiefs ni tofauti kwani katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini Premier Soccer League (PSL) imetwaa mara 13 tu.

Ligi ya Afrika Kusini ilianza rasmi mwaka 1971 ikifahamika National Professional Soccer League (NPSL) hadi 1984 ambapo Kaizer ilitwaa mataji matano kuanzia 1974, 1977, 1979, 1981 na 1984.

Mnamo mwaka 1985 ilibadilishwa tena jina na kuitwa National Soccer League (NSL) hadi 1995 ambapo katika kipindi hicho miamba hiyo ilitwaa jumla ya makombe matatu tu kuanzia 1989, 1991 na 1992.

Mwaka 1996 ikabadilishwa tena jina na kuitwa Premier Soccer League (PSL) linaloendelea kutumika hadi sasa, Kaizer imetwaa mataji manne tu kuanzia msimu wa 2003/04, 2004/05, 2012/13 na 2014/15.

Lakini ni klabu yenye makombe mengi nje ya Ligi Kuu ikiwa na jumla 41, yakiwamo 13 ya Kombe la Taifa (Nedbank Cup) ikishikilia rekodi kama ilivyo kwa Kombe la Ligi (Telkom Knockout, huku ikibeba MTN 8 (Top 8 Tournament) mara 15 ikiwa pia ni rekodi katika michuano hiyo, wakati kwenye michuano ya kimataifa imebeba Kombe la Washindi Afrika mwaka 2001.

Imefika fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2020-2021 na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco na mwaka 2002 ilicheza CAF Super Cup na kupoteza pia. Mwaka 2001 ilishinda tuzo ya Klabu Bora ya Afrika ya Mwaka.

NAFASI YA TANO

Katika Ligi ya kwao msimu uliopita Kaizer ilimaliza ikiwa nafasi ya tano baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 44 kufuatia kucheza michezo 30 ambapo ilishinda 13, sare mitano na kupoteza 12.

FAINALI YA SIMANZI

Kaizer ilitwaa Kombe la Washindi 2001 kabla ya michuano hiyo haijaunganishwa na KOmbe la CAF mwaka 2004 kuwa Kombe la Shirikisho baada ya kuifunga Inter de Luanda ya Angola jumla ya mabao 2–1.

Licha ya furaha kukithiri kutokana na ubingwa huo, mwishowe ilileta majonzi baada ya mashabiki wa soka 43 wa Afrika Kusini kupoteza maisha katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Ellis Park.

MASTAA WAO

Kaizer imesheheni mastaa wengi wakali ila miongoni mwa jina kubwa ambalo mashabiki wengi wa soka wanapenda kuliona wakati wa mchezo baina ya miamba hii ni la mshambuliaji, Ranga Chivaviro.

Nyota huyo aliyejiunga na Kaizer akitokea Marumo Gallants iliyoshuka daraja, alionyesha kiwango kizuri msimu uliopita hasa mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hivyo kuzivutia timu nyingi.

Chivaviro aliwindwa sana na Yanga iliyomuhitaji kwa ajili ya msimu ujao kutokana na kiwango bora alichokionyesha alipofunga mabao sita ya CAF nyuma ya Fiston Mayele aliyeibuka kidedea na saba.

Timu hii imewahi kutumikiwa na mastaa waliotamba katika soka la Afrika na nje ya mipaka ya bara hilo akiwamo, manahodha Neil Tovey na Lucas Radebe, Gary Bailey, John 'Shoes' Moshoeu, Shaun Bartlett, Steve Komphela, Siyabonga Nomvete na Doctor Khumalo.

Amakhosi wataitibulia Yanga sherehe ama watageuzwa asusa wa pati la Wiki ya Mwananchi? Subiri tuone baada ya dakika 90 za pambano hilo litakalopigwa kwa Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: