Vichwa vya habari vya vyanzo mbalimbali vya habari za michezo juma hili viligubikwa na habari ya uhamisho wa mchezaji wa klabu ya Young Africans kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Fiston Kalala Mayele.
Hadi sasa taarifa zinasema mchezaji huyo ameuzwa kwenye klabu tajiri ya Pyramids inayocheza ligi kuu ya Misri. Akiwa na Yanga, Fiston Mayele ameshinda misimu miwili ya ligi kuu Tanzania bara,misimu miwili ya kombe la shirikisho, ASFC, Ngao ya Jamii na pia medali ya mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho la Afrika.
Mayele binafsi ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu,mfungaji bora mwenza wa msimu na pia Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mlolongo wa mafanikio kupitia klabu na mafanikio binafsi ya Mayele yanaweza kueleza kwa nini uhamisho wake uongelewe sana si hapa Tanzania bali Afrika nzima na nje ya mipaka. Baada ya mafanikio vilabu barani Afrika na Asia viliandamana vikipiga hodi kwenye klabu ya Yanga vikitafuta kupata saini ya mchezaji huyo nguli.Unaweza kusema Yanga imeponzwa na mafanikio yake.
Kumbuka hii inatokea Yanga ikiwa imeshaagana na kocha aliyekuwa sehemu ya mafanikio yao mtunisia Nasredeen Nabi ambaye tayari nafasi yake imechukuliwa na Muargentina Miguel Gamondi.
Ni kawaida timu zinapofika kilele cha mafanikio kama kucheza fainali hujikuta katika hali ya wachezaji na hata maafisa wa benchi la ufundi kuwindwa na klabu nyingi zenye msuli wa fedha na kiu ya mafanikio.
Fainali ya Ligi ya Mabingwa kati ya FC Porto ya Ureno na Monaco ya Ufaransa ulishuhudia klabu hizo ambazo si tajiri sana Ulaya zikipoteza rasilimali watu muhimu kama kocha Jose Mourinho wa Porto na mshambuliaji Didier Drogba wa Monaco walionyakuliwa na Chelsea ya London.
Kwa hapa nchini,wako wengi sana waliopenda Mayele aondoke Yanga hasa wale mahasimu wa Yanga huku wengi sana walio wapenzi wa Yanga wakipiga mkesha wa maombi asiondoke.Pamoja na tofauti hizo zilizo kama mchana na usiku, jambo moja pande mbili hizi zinakubaliana ni nafasi ya Mayele katika timu ya Yanga katika misimu yake miwili pale mitaa ya Twiga na Jangwani. Waliomchukia walifanya hivyo kutokana na umuhimu wake na mchango wake kwa Yanga na waliompenda kadhalika walisukumwa na umuhimu wake na mchango wake kwa Yanga.
Ni hilo basi, mengine ikiwa ni pamoja na stahili yake ya kushangilia, maarufu kama kutetema ilikuwa ni bonasi. Mchezo wa mpira wa miguu huamuliwa na magoli,mayele aliamua michezo mingi ya yanga kwa magoli pale yalipohitajika. Yanga ilishinda michezo yake kwa tofauti ya magoli lakini ilishinda pale ilipohitajika. Jambo tunaloweza kusema kuwa ilikuwa ni bahati au mkakati wa benchi la ufundi ni jinsi Mayele alivyokuwa na mwendelezo na hakupata majeraha mabaya katika misimu miwili ya ligi ambayo amefunga mabao 33.
Unajiuliza kama Mayele angepata majeraha mabaya hasa mwanzoni mwa msimu kabla ya ujio wa Kenny Musonda kwenye dirisha dogo hali ya wananchi ingekuwaje?Unajiuliza kama yaliyomtokea Mzambia Phiri pale Simba yangemtokea Mayele ubingwa ungekuwepo? Ukiangalia Yanga ilikuwa na vikosi vipana lakini mstari wa umaliziaji ulimtegemea Mayele kwa kiasi kikubwa.
Ukiangalia mahasimu wao Simba, kwao mabao yalitokea kokote. Yalitokea kokote ndiyo maana hata mabao ya mfungaji mwanzo Saido Ntibazonkiza hayakupewa thamani ileile kama yale ya Mayele.
Haishangazi kuona kwamba Yanga walimchukulia Mayele kama mchezaji wa kipekee kwenye timu yao kwa sababu hawakumjua mfungaji mwingine. Hata walipomleta mshambuliaji wao hatari wa zamani Haritier Makambo bado alionekana kama bunduki iliyopata kutu.
Hali hii ya kuwa na wigo mwembamba upande wa wamaliziaji sidhani hata kama kocha Nabi angelikuwepo angekubali kuingia msimu wa tatu na presha ya kumtegemea mshambuliaji mmoja Mayele.
Lazima Yanga wangeingia sokoni kutafuta mshambuliaji namba tisa wa kiwango cha Mayele au vinginevyo wangetafuta mawinga au viungo wa ushambuliaji wenye kufikisha angalau bao 10 kwa msimu. Hadi sasa naamini Yanga wako kwenye presha tena kubwa sana ya kupata mchezaji au wachezaji wa kurithi majukumu ya Mayele wa kufunga mabao.
Bila shaka Mayele amefaidika na mafanikio yake au tuseme juhudi zake pale Jangwani, kwani klabu anayojiunga nayo si klabu inayotegemea aibebe mabegani uwanjani, ingawa presha ya kuonyesha kwamba kuwa mmoja wa wafungaji bora wa ligi za ndani Afrika hakubahatisha. Na upande wa mfukoni ,mambo yake yamefika mahali pazuri.
Mahali ambapo wanasoka wengi wanapenda kufikia kama wachezaji wa kulipwa. Kila la kheri Mayele 'Mzee wa Kutetema'. Yanga watakukumbuka Ligi Kuu itakukumbuka na watanzania watakukumbuka.