Kiungo Mshambuliaji wa Yanga, Farid Mussa Malick amefichua siri ya alichoambiwa na Kocha Msaidizi Cedrick Kaze kabla ya kuingia kuchukua nafasi ya Mudathir Yahya Abbas katika mchezo wa mwisho wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya TP Mazembe.
Timu hizo zilikutana juzi Jumapili (April 02) mjini Lubumbashi katika Uwanja wa TP Mazembe na Young Africans kuchomoza na ushindi wa 1-0, lililofungwa na kiungo huyo.
Farid amesema wakati akijiandaa kuingia kipindi cha pili Kocha Kaze alimsisitiza kuwasoma mabeki wa TP Mazembe, ili kupata nafasi ya kuisaidia timu kupata bao kutokana na udhaifu wao.
Amesema alifanya alichoagizwa na Kocha na kwa bahati nzuri alipata nafasi ya kipekee kufuatia makosa ya Mlinda Lango wa TP Mazembe kuutema mpira, na alichokifanya ni kufunga kwa utulivu bao ambalo liliipa ushindi Yanga na kufikisha alama 13 katika msimamo wa Kundi D.
“Nilipokuwa benchi kocha alinisisitiza kuwasoma mabeki wao huku akinisisitiza pia kuwa kwa asilimia kubwa ni wachezaji ambao hawakuwaona mchezo wa kwanza hivyo baada ya kupata nafasi na wao waliingia kuonyesha walichonacho ndio ugumu tuliokutana nao”
“Bao nililofunga lilikuwa linahitaji maamuzi ya haraka kama nilivyofanya kwani ulikuwa ni mpira wa kutemwa na sio makosa ya mabeki nilipoipata hiyo nafasi sikutaka kufanya mambo mengi nilijiweka sawa na kukwamisha mpira nyavuni na nashukuru ndilo lilikuwa bao la ushindi,” amesema Farid
Farid amesema anafurahi kuwa mmoja wa wachezaji ambao wameifikisha timu kwenye malengo waliyojipangia baada ya kutinga hatua ya makundi kuhakikisha wanafanya vyema na kucheza hatua ya Robo Fainali.
Amesema baada ya kutinga hatua hiyo, wao kama wachezaji malengo ni kuona wanacheza fainali ya mashindano hayo huku akiweka wazi kuwa hilo linawezekana kutokana na ubora wa kikosi chao na chachu ya mafanikio waliyonayo wao kama wachezaji.
Mbali na Young Africans timu nyingine zilizofuzu hatua ya Robo Fainali kwenye Shirikisho ni Asec Memosas, AS FAR. Marumo, Rivers United, USM Algiers na Pyramids.
Kati ya hizo Young Africans inaweza kupangwa na Pyramids (Misri), Rivers United (Nigeria) au USM ya Algeria.