Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ni kama amewashawasoma wapinzani wake Simba kuelekea katika mchezo wa Watani wa Jadi kufuatia kuamua kumpa majukumu mazito beki mpya wa timu hiyo, Ibrahim Ahmad ‘Bacca’ ya kuhakikisha hakuna mshambuliaji yeyote wa Simba anayeweza kupenya na kufunga bao.
Safu ya ushambuliaji ya Simba iko moto kwa sasa ikiongozwa na Jean Baleke ambaye amefunga mabao matano kwenye mechi mbili zilizopita.
Bacca kwa sasa amekuwa akipata nafasi ya kucheza baada ya kuonyesha uwezo mzuri kwenye michuano ya kimataifa jambo ambali limempa Imani kubwa Nabi kumtumia kwenye mchezo wa Dabi ya Kariakoo itakayopigwa leo Jumapili hiii Dimba la Mkapa.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo zinadai kuwa, Nabi ameanza kufanya maandalizi ya kumuandaa beki huyo ili aanze kwenye mchezo huo kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa kila anapopata nafasi.
“Mwalimu amekuwa akifanya maandalizi ya kufanya mabadiliko hasa katika safu ya ulinzi kwa kuhakikisha wanapata ingizo jipya ili kuifanya timu kuwa imara, Bacca ameonekana kuaminiwa katika nafasi kubwa ya kuanza katika mchezo wa Jumapili,” alisema mtoa taarifa.
Baada ya kumtafuta Nabi azungumzie ishu hiyo ambapo alisema ana mpango wa kufanya mabadiliko katika sehemu kubwa ya kikosi chake ikiwemo safu ya ulinzi lakini aligoma kuingia kiundani zaidi.
“Tunafanya maandalizi kulingana na aina ya mchezo ambao tunaenda kucheza ndiyo maana tumekuwa na timu ambayo imekuwa inabadilika kila wakati, mabadiliko yatakuwepo kwenye maeneo mengi ikiwemo hilo safu ulinzi ingawa siyo sawa kutaja nani atakuwepo,” alisema Nabi.