Straika wa zamani wa Nazareth, Simba na Taifa Stars, Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ amemwangalia mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize na kutamka kuwa dogo anajua sana.
Mzize amekuwa katika kiwango bora na aliisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC).
Katika mchezo huo, Mzize alifunga mabao mawili dakika za 70 na 88, kinda huyo aliingia uwanjani kipindi cha pili dakika ya 45 kuchukua nafasi ya Jesus Muloko.
Nguli huyo wa zamani alisema Mzize ni mshambuliaji bora ambaye amekamilika kila idara, hivyo Watanzania wanatakiwa kukilinda kipaji chake kwa kutomkatisha tamaa kwa kumzomea pindi anapokosea.
“Nchi ina uhaba wa namba tisa sasa amepatikana, tumlinde kwa nguvu zote, tusimzomee, anatakiwa kuwa na mwendelezo wa kile anachokifanya na mwendelezo unapatikana kwa kupata dakika za kutosha.
“Nimefuatilia pasipo na shaka anatakiwa kuwepo timu ya Taifa, hata kwa kukaa nje ili tuendelea kumtengenezea mazingira ya kujiamini.
“Hata kocha wa Stars aambiwe dogo anajua akichaguliwa atazidi kujiamini,” alisema Gabriel ambaye kwa sasa ni Meneje wa Fountain Gate FC inayoshiriki Ligi ya Championship.